RC Macha: Wenye  taarifa za waliofukiwa mgodini wazilete ofisini

Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha amefafanua kuhusu idadi ya waliokuwamo ndani ya shimo la mgodi ambao mwamba wake ulikatika na kusababisha vifo vya watu sita.

Akizungumza kwa njia ya simu na Mwananchi Digital leo Jumatatu ya Mei 19, 2025  kuhusu maendeleo ya ukoaji, Macha amesema ni kweli mgodi huo umesababisha vifo vya watu sita huku wengine 11 wakiokolewa, lakini hadi sasa hakuna taarifa zaidi.

Macha amesema hayo kufuatia taarifa zisizo rasmi kwamba bado kuna watu wengi wamefukiwa kwenye shimo hilo la mgodi wa dhahabu.

Kiongozi huyo alikuwa akizungumzia mgodi unaomilikiwa na kikundi cha Hapa Kazi Tu, uliopo Mwakityolo mkoani Shinyanga watu sita wamekufa na wengine 17 kufukiwa na kifusi. Ajali hiyo ilitokea Jumamosi ya Mei 17.

“Tulipofika eneo la tukio, baada ya kupata taarifa tulipowauliza watu waliokuwepo hapo idadi ya watu walioingia mgodini, kila mmoja alikuwa na idadi yake, kuna waliosema watu wasiozidi 20, wengine wakasema watu 17 na wengine wakasema watu 18.

“Wakati wa uokoaji tukawatoa watu 11 wakiwa hai na wengine sita wakiwa wamefariki dunia,  hivyo kufanya idadi kuwa watu waliokuwemo ndani ya shimo kufikia 17,” amesema Macha.

Hata hivyo, Macha amesema hawakuishia hapo bali waliwaomba wananchi wenye taarifa zaidi iwapo wanahisi kuna watu ndani ya shimo au hawaonekani kwenye jamii au familia watoe taarifa kwenye ofisi ya Mkuu wa Mkoa.

“Tulitoa nafasi na leo (Jumatatu) ni siku ya tatu maana tukio limetokea Jumamosi Mei 17 na leo ni Mei 19,2025  kwamba kama kuna mtu haonekani kwenye jamii au familia basi watoe taarifa,” amesema Macha.

Kwa mujibu wa Macha amemuomba mtu aliyejitambulisha kwa jina la Michael Mzibamziba akidai kwamba kuna jamaa zake bado wako chini na simu zao hazipatikani afike ofisi ya Mkuu wa Mkoa ili aweze kusaidiwa kuwatafuta kwa kwenda kuangalia upya kwenye mgodi huo.

Mzibamziba alinukuliwa na gazeti la Mwananchi akisema; “Hiki kitalu wachimbaji wanaofika asubuhi ni wengi sana, hawa waliookolewa ni wachache. Tunaomba uchunguzi zaidi ufanyike ili waliobaki chini waokolewe. Kuna jamaa zangu wako chini na tulikuwa tunawasiliana, sasa hawapatikani.”

Hata hivyo, Macha amesema mgodi huo ni shimo lililo wazi ambapo watu hao hawakuwa wakichimba bali walikuwa wakiokota mawe na wakati wakifanya hivyo mwamba ulikatika na kuwafunika.

“Mgodi wenye ni shimo ambalo hata mimi niliingia ni sehemu iliyo wazi wanakwenda kuokota mawe ndani. Bado milango yetu ipo wazi kwa yeyote ambaye anaona ndugu au jamaa yake hajaonekana na alikuwamo kwenye mgodi huo, tuko tayari kusaidiana naye kumtafuta,” amesema Macha.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *