RC atoa agizo maalumu kwa wakuu wa wilaya

Shinyanga. Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha ametoa agizo kwa wakuu wa wilaya za Shinyanga, Kahama na Kishapu kupitia vyuo vya kati mkoani humo kuhakikisha elimu ya amali inayotolewa vyuoni inajumuisha ufundishaji wa utengenezaji wa mizinga ya kisasa ya asali kwa vitendo.

Lengo ni kuongeza uzalishaji wa asali na kukabiliana na changamoto zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi.

Anamringi ameyasema hayo leo, Machi 5, 2025, katika hotuba aliyotoa kwenye hafla fupi ya kukabidhiwa vifaa vya kilimo vilivyotolewa na World Vision, kwa ajili ya mradi wa mbogamboga na uzalishaji wa asali wilayani Kishapu.

Katika hotuba hiyo, alimtaka Ofisa Kilimo wa Wilaya ya Kishapu kusimamia na kutunza vifaa hivyo vizuri.

“Lengo letu ni kuhakikisha wahitimu wanajua kutengeneza mizinga ya kisasa ya nyuki.

“Ninawaomba wakuu wa wilaya zote wasimamie hili kupitia vyuo vyetu vya kati, wanafunzi wapelekwe kwenye miradi hii na kujifunza kwa vitendo,” amesema.

Naye Mwakilishi wa World Vision Kanda ya Ziwa, Shukrani Dickson amesema kuwa vifaa vilivyokabidhiwa vina thamani ya Sh97 milioni, lengo likiwa ni kuhakikisha wakulima wanapata tija katika kilimo na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

“Vifaa hivi vinajumuisha mashine ya kukaushia mazao ili yasipoteze virutubisho, jenereta, vifaa vya kutolea asali, mbegu za mbogamboga (paketi 2,300), mizinga ya nyuki ya kisasa, seti ya pampu kwa ajili ya kumwagilia na mifuko 4,000 ya kuhifadhia mazao,” amesema Shukrani.

Amesema, “Vifaa hivyo vitatolewa kwa kata tatu katika Wilaya ya Kishapu, ambazo ni Mwamashele, Lagana, na Ngofila, ambapo ndiko iliko miradi ya mbogamboga na uzalishaji wa asali,” amesema Shukrani.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Peter Masindi amesema vifaa hivyo watavisimamia ili vilete manufaa kwa wananchi.

Mmoja wa wakulima kutoka kata ya Lagana, Joyce Nkwabi amesema, “ukame umekuwa ni changamoto kubwa kwenye kilimo cha mbogamboga, lakini kwa msaada wa vifaa zikiwamo pampu za kumwagilia, tunaamini zitatusaidia kutatua changamoto ya uhaba wa mbogamboga. Pia, suala la uzalishaji wa asali ni mradi tunaouanzisha kwa sasa,” amesema Joyce.