RC atishia kufunga biashara kisa uchafu

Pemba. Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba, Rashid Hadid Rashid amesema Serikali ya Mkoa huo itachukua hatua za kisheria dhidi ya wafanyabiashara watakaoshindwa kudumisha usafi katika maeneo yao ya kazi, ikiwemo kufungia biashara zao.

Kauli hiyo ameitoa leo Ijumaa Aprili 18, 2025, wakati wa operesheni maalum ya usafi wa mazingira iliyofanyika katika maeneo mbalimbali ya mji wa Chakechake, Kusini Pemba.

Wananchi wakishiriki operesheni maalumu ya kufanya usafi Mjini Chake Cheke ikiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Chakechake Mgeni Khatib Yahya aliyevalia mtandio rangi ya manjano.

“Hali ya usafi katika mji huu bado haijaridhisha. Maeneo mengi ni machafu, jambo linaloweza kusababisha majanga mbalimbali endapo hatua hazitachukuliwa kuboresha mazingira,” amesema mkuu huyo wa mkoa.

Amesema haikubaliki kwa mfanyabiashara kuendesha shughuli zake katika mazingira machafu, hasa katika kipindi hiki cha mvua kubwa, kuna hatari ya kuzuka kwa magonjwa ya mlipuko.

“Wapo baadhi ya wafanyabiashara wa vyakula kama supu na chipsi ambao hufanya biashara katika mazingira yasiyo safi, huku wananchi wakiendelea kupata huduma hizo bila kujali hali ya usafi. Hili haliwezi kuvumiliwa,” ameongeza.

Amesisitiza kuwa usafi ni tabia inayopaswa kujengwa na si suala la kusubiri Baraza la Manispaa kuingilia kati. Wafanyabiashara wanapaswa kuhakikisha maeneo yao ya kazi ni safi ili kuepusha madhara kwa jamii.

Katika kipindi hiki cha mvua, Mkuu huyo wa mkoa amewataka wafanyabiashara pamoja na wananchi kwa ujumla, kushirikiana ili kuhakikisha mji unakuwa safi na salama muda wote.

“Serikali ya Mkoa wa Kusini Pemba itawachukulia hatua wananchi na wafanyabiashara watakaopuuzia suala la usafi. Haiwezekani kuuza supu au chipsi katika mazingira machafu,” amesema.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Chakechake, Mgeni Khatib Yahya amewataka wafanyabiashara kuepuka kufanya shughuli zao katika maeneo yasiyo rasmi na badala yake kutumia masoko yaliyotengwa rasmi kwa ajili ya biashara.

Amesema pamoja na kuwepo kwa maeneo hayo maalumu, bado baadhi ya wafanyabiashara wameendelea kukaidi na kuendesha biashara pembezoni mwa barabara, jambo ambalo ni hatari kwa afya na usalama wa jamii.

Pia ameeleza kuwa baadhi ya wafanyabiashara hasa wa bidhaa za samaki wamekuwa wakifanya shughuli zao katika mazingira machafu bila kujali usafi.

Wananchi wakishiriki operesheni maalumu ya kufanya usafi Mjini Chake Cheke ikiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Chakechake Mgeni Khatib Yahya aliyevalia mtandio rangi ya manjano.

Baadhi ya wafanyabiashara waliohojiwa, akiwemo Haji Ali Makame, wamekiri kuwepo kwa changamoto ya baadhi ya wenzao kutokuzingatia usafi, hali inayohatarisha afya za wateja.

“Tunahitaji kuhamasishana juu ya umuhimu wa kudumisha usafi, kwa sababu kufanya biashara katika mazingira machafu ni hatari kwa afya,” alisema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *