
Dar es Salaam, Hatua ya Rayvanny kuanzisha Next Level Music (NLM) ilipokelewa na wengi kama rekodi lebo inayokuja kushindana vilivyo na hata kutikisa himaya ya WCB Wasafi yake Diamond Platnumz ambayo ndio ilimtoa kimuziki miaka minane iliyopita.
Lakini mambo yanaonekana kwenda ndivyo sivyo kwa mshindi huyo wa BET 2017, ikiwa ni miaka mitatu tangu kuanzishwa kwa NLM, bado huwezi kusema imeleta au itakuja kuleta ushindani mkubwa kwa WCB Wasafi.
Utakumbuka Rayvanny alitolewa na WCB Wasafi kupitia wimbo wake, Kwetu (2016) baada ya kuachana na Tip Top Connection ambapo alisota kwa muda mrefu huku akitoa wimbo mmoja tu, Upo Mwenyewe (2012).
Chini ya WCB Wasafi, Rayvanny alifanya makubwa na kuandika rekodi nyingi, mathalani ndiye msanii wa kwanza Tanzania na wa pili Afrika Mashariki kushinda BET, wa kwanza Afrika Mashariki kufikisha ‘streams’ milioni 100 katika mtandao wa Boomplay.
Ni msanii wa kwanza kutoka Afrika kutumbuiza katika tuzo za MTV Europe Music Awards (MTV E MAs), ni msanii wa kwanza Afrika Mashariki kwa albamu yake, Sound From Africa (2021) kufikisha ‘streams’ zaidi ya milioni 100 ndani ya wiki moja.
Pia ni msanii wa kwanza Tanzania kushika namba moja chati za Billboard Mexico Airplay kupitia wimbo, Mama Tetema (2021), ikiwa ni mara ya pili kuingia chati hizo baada ya hapo awali kutamba Billboard Top Triller Global Chart akiwa na Dj Cuppy wa Nigeria.
Ndiye msanii aliyetolewa na WCB Wasafi na kushinda tuzo nyingi za kimataifa, Rayvanny ameshinda tuzo kama BET (Marekani) 2017, Zikomo (Zambia) 2022, Afrimma (Marekani) 2022, EAEA (Kenya) 2022, DIAFA (Dubai) 2022 n.k.
Na kubwa zaidi, Rayvanny ni msanii wa kwanza kufungua lebo yake, Next Level Music (NLM) akiwa bado chini ya WCB Wasafi, wakati Harmonize na Rich Mavoko walifungua zao, Konde Music Worldwide na Billionea Kid baada ya kuondoka Wasafi.
Alifanya hivyo hapo Machi 2021 na kufikia Septemba 2021 akamtambulisha msanii wa kwanza wa NLM, Mac Voice ambaye alikuja na Extended Play (EP) yake, My Voice (2021) huku akimshirikisha Rayvanny katika nyimbo mbili.
Mac Voice na EP yake walipata mapokezi mazuri, kwa mfano ndani ya mwezi mmoja alisikilizwa (streams) zaidi ya mara milioni 1 huko Boomplay, kupata wafuasi (subscribers) 100,000 YouTube, pia akitazamwa (views) zaidi ya mara milioni 4 YouTube.
Rekodi nyingi ni kafikisha ‘streams’ zaidi ya milioni 10 kwenye mitandao ya iTunes, Spotify, Audiomack na Boomplay huku akiwania tuzo ya African Entertainment Awards USA (AEAUSA) kama Msanii Bora Chipukizi 2021.
Hata hivyo, baada ya mwaka 2021 kasi ya NLM na Mac Voice ameshuka sana ndani ya Bongo Fleva na sio kama ambavyo walitabiriwa kuja kutoa changamoto kwa WCB Wasafi ambao wamefanya vizuri kwa muda mrefu.
Wakati NLM ikiwa imemtoa msanii mmoja ndani ya miaka mitatu, WCB Wasafi wao ndani ya muda kama huo waliwasaini na kuwatoa wasanii watano ambao ni Harmonize (2015), Rayvanny (2016), Queen Darleen (2016), Rich Mavoko (2016) na Lava Lava (2017).
Haikuishia hapo bali waliongeza wasanii wengine ambao ni Mbosso (2018), Zuchu (2020) na D Voice (2023) ambaye alitambulishwa na albamu mpya, Swahili Kid (2023) ikiwa na nyimbo 10.
Baadhi ya wasanii wa WCB Wasafi walipata mapokezi mazuri kipindi cha mwanzo, mathalani Harmonize alishinda African Muzik Magazine Awards (AFRIMMA) 2016 kama Msanii Bora Chipukizi, tuzo ambayo pia Zuchu alikuja kuishinda 2020.
Lakini kwa upande Mac Voice haikuwa hivyo hadi sasa hajashinda tuzo yoyote kubwa, iwe ya ndani kama Tuzo za Muziki Tanzania (TMA) wala zile za USA (AEAUSA) kutoka Marekani ambazo alitajwa hapo awali.
Hata hivyo, ukweli utabaki kuwa NLM imewekeza sana kwa Mac Voice, Rayvanny amejitoa sana kwake wakiwa tayari wameshirikiana katika nyimbo tano ambazo ni Tamu (2021), Bora Peke Yangu (2021), Pombe (2021), Muongeze (2022) na Mwambieni (2023).
Hiyo ni sawa na Diamond alivyojitoa kwa Rayvanny, wawili hao wametoa nyimbo tisa pamoja ambazo ni Salome (2016), Iyena (2018), Mwanza (2018), Tetema (2019), Timua Vumbi (2019), Amaboko (2020), Woza (2020), Nitongoze (2022) na Yaya (2023).
Utakumbuka wimbo ‘Nitongoze’ ndio uliompa Rayvanny tuzo yake ya kwanza ya TMA.