Dar es Salaam. Lazima tukubali kwamba sio kila mwanamuziki anayefanya vizuri au mwenye nguvu ya ushawishi anaweza kuisimamia rekodi lebo na ikawa na matokeo makubwa katika tasnia, na ndicho kinaonekana kwa Rayvanny kwa sasa.
Lebo ya Rayvanny, Next Level Music (NLM) imekuwa tofauti kabisa na vile ilivyotarajia na wengi, hivyo sio vibaya iwapo ataamua hata kwa uchache kujifunza kwa mwimbaji wenzake, Nandy anayeisimamia The African Princess.
Utakumbuka Machi 2021 akiwa bado WCB Wasafi ndipo alikuja na NLM na kufikia Septemba akamtambulisha msanii wa kwanza, Mac Voice aliyetoka na EP yake, My Voice (2021) huku Rayvanny akishiriki katika nyimbo mbili.

Mac Voice alipata mapokezi mazuri, mathalani kwa mwezi mmoja tu alisikilizwa zaidi ya mara milioni 1 katika mtandao wa Boomplay, kutazamwa zaidi ya mara milioni 4 YouTube huku akipata wafuasi 100,000 katika jukwaa hilo.
Kwa ujumla kupitia EP yake, Mac Voice alisikilizwa zaidi ya mara milioni 10, zikiwa ni data kutoka mitandao ya Spotify, Audiomack, iTunes na Boomplay huku akiwania tuzo ya African Entertainment Awards USA (AEAUSA) kama Msanii Bora Chupukizi 2021.
Hata hivyo, tangu Rayvanny kuondoka WCB Wasafi Julai 2022, ukawa mwanzo wa Mac Voice kushuka katika Bongofleva na sasa ni zaidi ya miezi tisa bila kutoa wimbo wowote kitu kinachoacha maswali.
NLM ilitegemewa italeta ushindani kwa WCB Wasafi kupitia wasanii itakayowaini ila ndio hivyo hadi sasa ina msanii mmoja pekee na huyu mmoja anakaa kimya kimuziki kwa takribani mwaka mmoja kitu ambacho huwezi kukiona WCB.
Staa wa Bongofleva Diamond Platnumz alipoanza kusaini wasanii WCB miaka ya mwanzoni alifululiza akianza na Harmonize (2015), Rayvanny (2016), Queen Darleen (2016), Rich Mavoko (2016), Lala Lava (2017), Mbosso (2018), Zuchu (2020) na D Voice (2023).
Hicho ndicho mashabiki wengi walikuwa wanakiona pale ambapo Rayvanny alitangaza kuanzisha lebo yake ya NLM, na kutokana amekaa na Diamond kwa muda mrefu, basi mbinu zote za kibiashara anazijua ila imekuwa ndivyo sivyo.
Ni tofauti kabisa na kwa Nandy ambaye Januari 2023 ndipo lebo yake, The African Princess ilimtambulisha Yammi akiwa msanii wa kwanza kusainiwa huku akija na EP yake, Three Hearts (2023) yenye nyimbo tatu ambazo hakumshirikisha msanii yeyote.
Nandy ambaye alivutiwa na kipaji cha Yammi baada ya kumuona akiimba TikTok, hakutaka kuwepo katika EP ya Yammi ili kutoa nafasi kwa mashabiki kumsikia yeye pekee kitu ambacho Rayvanny alimnyima Mac Voice.
Tangu kutambulishwa 2023, Yammi amefanya vizuri kimuziki na kujizolea mashabiki zaidi ya milioni 1.2 Instagram wakati huo Mac Voice aliyetambulishwa 2021, hadi sasa akiwa na wafuasi 536,000 pekee.

Kibaya zaidi ni kwamba NLM wameshindwa kabisa hata kuuidhinisha (verified) ukurasa wa Mac Voice, huduma ambayo sasa hivi mtu yeyote yule anaiweza kuipata, ni fedha yako tu unajibebea blue tiki kutoka Meta!.
Kitu hicho huwezi kukiona WCB Wasafi, The African Princess hata Konde Music Worldwide ni NLM pekee – tena lebo inayosimamiwa na mshindi wa tuzo kubwa duniani – BET- aliyoshinda 2017 na hadi sasa akiwa msanii pekee Tanzania kufanya hivyo.
Wakati huo ambao mitandao ya kijamii imekuwa nyenzo muhimu kwa wasanii kutangaza kazi zao, huoni kitu hicho kwa Mac Voice, hii ni hatari kubwa sana kwake kipindi hiki ambacho ukubwa wa msanii inapimwa kwa idadi ya wafuasi alionao mtandaoni.
Mfano baada ya Diamond kumpiku Wizkid wa Nigeria kwa kuwa na wafuasi wengi Instagram, kuna mashabiki wanaamini kuwa Diamond ni mkubwa kimuziki kuliko Wizkid anayeuza zaidi mtandaoni na kushinda tuzo nyingi kubwa duniani.
Kudumaa kwa chapa ya Mac Voice kulionekana tangu mwanzo, mfano ni Rayvanny kuweka video zote mbili za nyimbo zao za awali, Tamu (2021) na Bora Peke Yangu (2021) katika chaneli yake ya YouTube kitu ambacho hukipo kwa Nandy wala Diamond.
Kosa lingine kubwa wanalofanya NLM kwa Mac Voie, ni kumfungia ndani sanaa msanii wao, msanii haonekani katika matukio makubwa na muhimu, hata alipokuwa akifanya vizuri alikuwa haonekani katika show mara kwa mara.
Wakati Mac Voice ‘akifungiwa ndani’ mwenzake Yammi anapita huku na kule akifanya shoo, keshatumbuiza huko Kenya mara kibao tena bila kuongozana na Nandy, na hata hapa Bongo anafanya shoo nyingi hata zile za kijamii akiwa peke yake.
NLM wakiendelea na mwendo huu wa kukaa miezi tisa bila kutoa wimbo mpya atapotea kabisa, kila siku wanakuja wasanii wapya, mfano tangu 2021 walipotoka Mac Voice, wamekuja wasanii wengi wanaofanya vizuri kama Chino Kidd, Yammi, Abigail Chams, D Voice n.k.