
Dar es Salaam. Licha ya jitihada zilizofanywa na Serikali, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na uongozi wa Klabu ya Simba, mchezo wa fainali ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika kati ya Simba na RS Berkane ya Morocco uchezwe kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, ngoma imekuwa ngumu kupindua meza.
Taarifa iliyotolewa na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Zubeda Sakuru leo Jumatatu Mei 19, 2025 imeeleza kuwa juhudi za mchezo huo kufanyika kwa Mkapa zimegonga mwamba hivyo, fainali ya pili itachezwa kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar, kufuatia uamuzi wa Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF).
“Tunaomba mashabiki na wapenzi wetu kuwa watulivu katika kipindi hiki,” amesema Sakuru katika taarifa hiyo.
Katika hatua nyingine, Simba imetangaza kuwa itatoa taarifa rasmi kuhusu maandalizi ya mchezo huo na namna mashabiki wake watakavyoshiriki kupitia mkutano maalum utakaofanyika kesho, Mei 20, 2025 saa 5 asubuhi katika ofisi za klabu hiyo zilizopo Oysterbay, jijini Dar es Salaam.
Mchezo huo wa fainali unatarajiwa kuchezwa Mei 25, 2025, ambapo katika mchezo wa kwanza nchini Morocco, Simba ilikubali kichapo cha mabao 2-0 mbele ya Berkane, hivyo kubaki na kibarua cha kupata ushindi wa zaidi ya mabao matatu ili kubeba taji hilo.