Dar es Salaam. Kiungo wa Yanga Khalid Aucho sasa ni rasmi atakuwa nje kwa takribani wiki tatu baada ya kuumia nyama za paja.
Jana wakati Yanga ikishinda nyumbani 1-0 dhidi ya Coastal Union,Aucho alilazimika kucheza mechi hiyo kwa dakika 45 hadi alipoomba kutoka baada kusikia maumivu kisha kutolewa na nafasi yake kuchukuliwa na mwenzake Mudathir Yahya.
Kiungo huyo amefanyiwa vipimo leo ambapo imegundulika atakuwa nje kwa wiki tatu taarifa ambayo imetolewa na klabu yake ya Yanga.

Kukaa nje kwa wiki tatu Aucho atazikosa mechi tatu kuanzia mchezo wa Azam utakaopigwa Aprili 10.
Mechi zingine atakazokosa ni ile ya ugenini dhidi ya Fountain Gate Aprili 20 pia mchezo wa nyumbani Yanga itakapowakaribisha Namungo ya Lindi Mei 13.
Hata hivyo Yanga bado Ina watu ambao wanaweza kuziba nafasi ya Mganda huyo, italazimika kuwatumia viungo wake Mudathir Yahya, Duke Abuya, Jonas Mkude na Aziz Adambwile ambao wanaweza kucheza nafasi hiyo ya Aucho.