
Dar es Salaam. Wakati kocha mpya wa Yanga Sead Ramovic akitarajiwa kukutana na mastaa wake wa kikosi cha kwanza leo, imefahamika kwamba benchi lake jipya litakuwa na sura moja mpya pekee huku uongozi ukimkabidhi watu watano wa kumsaidia.
Ramovic atakutana na kikosi cha timu hiyo kesho ambacho kina mastaa ambao hawakuitwa timu za Taifa akiwemo Stephene Aziz KI pamoja na Pacome Zouazoa kwa ajili ya utambulisho maalumu ambapo hapohapo ataanza ratiba ya mazoezi kwa ajili ya kujiandaa na mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi dhidi ya Al Hilal.
Kocha huyo raia wa Ujerumani aliyechukua nafasi ya Muargentina Miguel Gamondi benchi lake la ufundi litakuwa na mtu mpya mmoja pekee ambaye atakuwa kocha msaidizi raia wa Serbia.
Ingawa Mwananchi halijapata jina lake lakini tayari kocha huyo ameshawasili nchini akisubiri utambulisho pekee ambao ulitarajiwa kufanywa na uongozi wa Yanga kuanzia jana na atatambulishwa rasmi.
Wasaidizi wa Gamondi wabaki
Yanga baada ya kumuondoa Gamondi na msaidizi wake wa kwanza Moussa Nd’ew haikutaka kulibadili sana benchi lao likibakiza wengine wote ambao watasaidiana na kocha mpya.
Watu watakaosalia kwenye benchi hilo ni kocha wa viungo Taibi Lagrouni na kocha wa makipa Alaa Meskini wote raia wa Morocco ambao walikuja baada ya kuajiriwa kwa Gamondi.
Taarifa kutoka ndani ya Yanga zinasema wawili hao wamebakizwa kufuatia kutoonekana na shida yoyote, lakini pia uongozi wa Yanga umeangalia msaada wao waliouonyesha kwenye timu hiyo kwa kipindi chote walichokaa hapo.
Pia, mchambuzi wa mikanda ya video atasalia Mpho Maruping raia wa Afrika Kusini wakati meneja wa timu atabaki Walter Harrison anayetumikia adhabu ya kusimamishwa na Kamati ya usimamizi ya Ligi Kuu.
Kitengo Cha matibabu nacho kitaendelea kusalia na wataalamu wale wale chini ya daktari Mosses Etutu huku Mtunza vifaa akiwa Mohammed Omar maarufu kwa jina la Mpogoro.
Moalin apewa cheo
Aliyekuwa kocha wa KMC, mwenye asili ya Somalia Abdihamid Moalin amepewa nafasi mpya ndani ya Yanga akienda kuwa Mkurugenzi wa Ufundi nafasi ambayo ilikuwa haina mtu kwa miaka mingi.
Yanga mara ya mwisho kuwa na Mkurugenzi wa Ufundi alikuwa Mholanzi Hans Van Pluijm aliyeshika nafasi hiyo kwa miezi sita pekee wakati akitolewa kuwa kocha mkuu wa timu hiyo nafasi yake ikienda kwa Mzambia George Lwandamina.
“Moalin hiki ndiyo cheo alichoambiwa kuanzia mwanzo, atakuwa Mkurugenzi na tunaamini kuwa anaweza kufanya kazi nzuri sana kwa kipindi atakachokuwa hapa ana uwezo wa juu sana,” kilisema chanzo.