Ramovic asimulia chanzo bifu lake na Aziz KI, Chama

Dar es Salaam. Aliyekuwa kocha wa Yanga, Sead Ramovic amevunja ukimya akiwa Algeria kwa kuzungumzia kilichomfanya aachane ghafla na mabingwa hao wa kihistoria nchini.

Kocha huyo raia wa Ujerumani ameinoa Yanga kwa miezi miwili na ushei kabla ya kufanya maamuzi hayo magumu, akiwa ameiongoza timu hiyo katika michezo 13 ya mashindano yote, ikiwamo sita za Ligi Kuu Bara alizoshinda zote, sita nyingine za Ligi ya Mabingwa Afrika na moja ya Kombe la Shirikisho.

Licha ya kuiwezesha Yanga kusalia kileleni mwa msimamo wa Ligi ikiwa juu ya Simba ikikusanya pointi 45, Ramovic alishindwa kuivusha timu hiyo kwenda robo fainali baada ya kutolewa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika wiki chache zilizopita.

Ramovic aliwaacha wadau wengi midomo wazi baada ya kuachana na Yanga, huku akijiunga na klabu ya CR Belouizdad ya Algeria.

Kocha huyu mwenye misimamo mikali alijiunga na Belouizdad muda mfupi baada ya kuandika barua ya kujiuzulu siku moja kabla mchezo wa ligi dhidi ya KenGold.

Baada ya kuondoka kwake kwa mujibu wa taarifa za ndani pamoja na mambo mengine inaelezwa kuwa kocha huyo mwenye umri wa miaka 45 alikuwa katika migogoro ya mara kwa mara na baadhi ya wachezaji wake, akiwemo Stephane Aziz Ki na Clatous Chama.

Hata hivyo, Ramovic ameamua kumaliza ukimya huo na kujitetea kuhusu uamuzi wake wa kuondoka Yanga, akieleza kuwa alitaka kushindana katika ligi kubwa zaidi.

“Kama kocha, unaishi kwa ajili ya nyakati kama hizi. Uamuzi wa kuondoka Yanga haukuwa rahisi, lakini nafasi bora ilijitokeza, na kuhamia CR Belouizdad ni fursa ambayo siwezi kuikataa. Ligi hii niliyoiweka mbele sasa nchini Algeria, unacheza kila wiki dhidi ya wapinzani wa kiwango cha juu, na hili ndilo nilitaka kama kocha,” alisema Ramovic katika mahojiano na Metro FM.

“Yanga ni klabu bora kabisa nchini Tanzania; kweli kuna timu tatu tu zinazoshindania ligi nchini Tanzania, ambazo ni Young Africans, Simba SC, na Azam FC.”

“Kwenda CR Belouizdad ni kutokana na mimi kutaka kujitahidi zaidi kama kocha na kutaka kuboresha ufanisi wangu. Hakuwa na uhusiano wowote na pesa au madai ya mgogoro na wachezaji.”

“Niliamua hili kwa ajili yangu mwenyewe ili kuwa sehemu ya timu bora Afrika, lakini nilijua maneno ya kijinga yangetokea kuhusu kwa nini niliondoka Yanga, lakini siyajali,” aliongeza Ramovic.

Ramovic alitua Yanga Novemba 15 mwaka jana akitokea TS Galaxy ya Afrika Kusini kuziba nafasi ya Miguel Gamondi aliyetimuliwa baada ya kupoteza mechi mbili mfululizo za Ligi Kuu dhidi ya Azam na Tabora United ilizoifunga 1-0 na 3-1 mtawalia, licha ya awali kuiongoza katika mechi nane mfululizo ikishinda bila kuruhusu nyavu kuguswa na kuivusha makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa msimu wa pili mfululoizo baada ya awali kuipeleka hadi robo fainali msimu uliopita.