Ramovic afichua kilichomzuia Ikangalombo

Dar es Salaam. Kocha wa Yanga, Saed Ramovic amesema kuwa mshambuliaji wa timu hiyo, Jonathan Ikangalombo ni mgonjwa ndiyo maana akashindwa kucheza mchezo wa Kombe la FA juzi.

Yanga ambao ni mabingwa watetezi iliibuka na ushindi wa mabao 5-0 na kufanikiwa kufuzu kwa hatua ya 32 ya kombe hilo, hata hivyo mashabiki wengi waliojazana kwenye Uwanja wa KMC Complex walishtuka kutomuona nyota huyo uwanjani.

Ikangalombo alisajiliwa na Yanga kwenye kipindi cha dirisha dogo lililofungwa Januari 15, mwaka huu akitokea AS Vita Club ya kwao DR Congo, huku akibeba matumaini makubwa ya kikosi hicho.

Akizungumza na Mwananchi, Kocha wa Yanga, Sead Ramovic alisema alishindwa kumtumia mchezaji huyo kwa kuwa alikuwa na changamoto ya kiafya, ingawa anaendelea vizuri na anaweza kurejea mazoezini muda wowote.

“Najua kiu ya mashabiki, asingeweza kucheza, alipata homa kali karibu wiki nzima na juzi ndio ameanza kuwa sawa, hakukuwa na ulazima wa kumlazimisha kucheza hii mechi (dhidi ya Copco),”

“Tutamuona maendeleo yake zaidi Jumatatu (leo), tutakapoendelea na mazoezi, hajafanya mazoezi vizuri na timu nzima tangu amefika na sasa amepata hiyo shida ya afya, tunaamini bado anatakiwa kuendelea kuwa sawa,” alisema kocha huyo ambaye aliiongoza Yanga kwenye mchezo wa kwanza wa Kombe la FA msimu huu.

Aidha Ramovic aliwashusha presha mashabiki wanaomsubiri nyota huyo,  akisema anahitaji kuingia kwenye mifumo ya timu yake taratibu na baada ya hapo ataonekana uwanjani.

“Kuna kazi tunatakiwa kuifanya kwake (Ikangalombo), huyu ni mchezaji mpya ambaye alifika hapa tukiwa kwenye mechi ngumu za Ligi ya Mabingwa Afrika, tunataka kwanza kumuona jinsi ambavyo ataunganika na wenzake na kuwa tayari kwenye falsafa za soka tunalotaka hapa.”

Mkongomani huyo ambaye ameitumikia timu yake ya taifa kwenye michezo miwili, anatajwa kama mmoja kati ya wachezaji wanaoweza kuisaidia Yanga kutetea tena ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu.

Kwa sasa Yanga ipo nafasi ya pili kwenye msimamo ikiwa na pointi 39, baada ya kucheza michezo 15 ambapo inaingia tena uwanjani Februari Mosi kuvaana na Kagera Sugar ukiwa ni mchezo wao wa kwanza wa mzunguko wa pili, utakaopigwa kwenye Uwanja wa KMC Complex Mwenge jijini Dar es Salaam.

Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza baina ya timu hizo uliopigwa Uwanja wa Kaitaba Agosti 29, mwaka jana, Yanga ilishinda mabao 2-0, yaliyofungwa na Maxi Mpia Nzengeli dakika ya 25 na Clement Mzize dakika ya 89.