Rais wa Somalia anusurika kifo bomu la Al Shabab

Mogadishu. Kundi la Al Shabab nchini Somalia limekiri kuhusika kwenye shambulio la bomu lililomlenga Rais wa nchi hiyo, Hassan Sheikh Mohamud.

Kwa mujibu wa Reuters tukio hilo limetokea Machi 18, 2025 ambapo wanamgambo hao walishambulia msafara wake wakati ulipokuwa ukienda uwanja wa ndege Mogadishu.

Taarifa za maofisa waandamizi wa Serikali na jeshi wameiambia Reuters Mohamud yuko salama baada ya shambulio hilo, na mshauri wa Rais Zakariye Hussein aliandika kwenye X kuwa, ‘yupo salama na anaendelea na safari yake’.

Wanajeshi na wakaazi wa eneo hilo walioshuhudia shambulio hilo walithibitisha kuwa msafara wa Rais ulikuwa umelengwa.

Mwandishi wa Reuters aliyekuwepo kwenye eneo la tukio aliona miili ya watu wanne waliouawa katika shambulio hilo karibu na Ikulu.

“Wapiganaji wetu walilenga msafara wa magari yaliyombeba Mohamud wakati walipokuwa wakiondoka Ikulu kuelekea uwanja wa ndege,” Al Shabaab ilisema kwenye taarifa iliyochapishwa katika kituo chao cha Telegram kinachohusiana na Al Qaeda.

Ingawa Al Shabaab mara kwa mara hufanya mashambulizi nchini Somalia kama sehemu ya kampeni yao ya muda mrefu ya kuipindua Serikali, shambulio la Jumanne lilikuwa la kwanza kumlenga moja kwa moja Mohamud tangu 2014, alipokuwa katika muhula wake wa kwanza, wakati walipolipua hoteli aliyokuwa akihutubia.

“Shambulizi hilo lilidhibitiwa huku Rais akiwa salama salimini,” taarifa iliyotolewa na Wizara ya Habari ya Somalia. Kulingana na Wizara hiyo, shambulio lilitokea katika wilaya ya Xamar-Jajab jijini Mogadishu.

Rais Mohamud ni nani

Sheikh Mohamud ameongoza taifa hilo kuanzia 2012, hadi sasa na ametumia muda mwingi wa maisha yake kama mwalimu, akifundisha katika shule na vyuo vikuu kadhaa, kwa mujibu wa BBC.

Kabla ya kuwa Rais wa Somalia, alikuwa mwanachama wa mashirika ya kiraia na alifanya kazi nchini Somalia wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Hassan Sheikh alizaliwa mwaka 1955 katika wilaya ya Jalalaqsi mkoa wa Hiraan nchini Somalia. Alipata elimu yake ya msingi katika mji aliozaliwa, alihudhuria shule ya sekondari na chuo kikuu huko Mogadishu.

Alihitimu kutoka Chuo Kikuu cha Teknolojia mwaka 1981. Baadaye alisoma katika chuo kikuu nchini India.

Aliporejea Somalia, Sheikh Mohamud alifanya kazi katika Wizara ya Elimu ya Somalia, akifundisha shuleni na vyuo vikuu. Mbali na ufundishaji na ustadi wake wa kisiasa, pia ni mfanyabiashara aliyejiajiri.

Mnamo Agosti 2012, Hassan alikua mjumbe wa Bunge la Shirikisho la wakati huo la Somalia.

Mnamo Septemba 10, 2012, wajumbe wa Baraza la Watu wa Bunge la Shirikisho la Somalia walimchagua Hassan Sheikh Mohamud kuwa rais wa nchi hiyo baada ya  uchaguzi usio wa moja kwa moja.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *