Rais wa Namibia kufanya ziara ya siku mbili Tanzania

Dar es Salaam. Rais wa Namibia, Netumbo Nandi-Ndaitwah anatarajia kuwasili nchini Tanzania kwa ziara ya siku mbili kuanzia kesho Mei 20 hadi 21, 2025, kufuatia mwaliko wa Rais Samia Suluhu Hassan.

Ziara hiyo itakuwa ya kwanza kwa Rais Nandi-Ndaitwah tangu aapishwe kuwa Rais wa Namibia Machi 21, mwaka huu, na inalenga kuimarisha uhusiano kati ya mataifa hayo mawili katika nyanja za kisiasa, kiuchumi, kijamii pamoja na elimu na uwekezaji.

Tanzania na Namibia zimekuwa na ushirikiano wa muda mrefu unaotokana na historia ya ukombozi barani Afrika, ambapo ziara hii inatarajiwa kufungua ukurasa mpya wa ushirikiano utakaoleta manufaa ya kiuchumi kwa wananchi wa pande zote mbili.

Akiwa nchini, Rais Nandi-Ndaitwah atapokelewa Ikulu na mwenyeji wake, Rais Samia, ambapo viongozi hao wawili watafanya mazungumzo ya ana kwa ana kabla ya kuongoza mazungumzo rasmi baina ya nchi hizo mbili, na hatimaye kuzungumza na wanahabari.

Mbali na mazungumzo hayo, Rais Nandi-Ndaitwah pia atatembelea Kituo cha Urithi wa Ukombozi wa Afrika pamoja na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ambapo anatarajiwa kutoa heshima kwa mchango wa Tanzania katika harakati za ukombozi, sambamba na kuhimiza ushirikiano wa kielimu na kiutamaduni kati ya Namibia na Tanzania.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *