Rais wa Jamhuri ya Namibia, Dk Netumbo Nandi-Ndaitwah amewasili nchini leo Mei 20, 2025 kwa ajili ya kuanza ziara rasmi ya siku mbili.
Ziara hiyo ya kwanza kwa Nandi-Ndaitwah kufanyika hapa nchini tangu kuingia kwake madarakani Machi 2025, inafuatia mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.

Baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, Dk Nandi-Ndaitwah amepokelewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo.
Akiwa nchini pamoja na mambo mengine, Nandi-Ndaitwah atafanya mazungumzo ya faragha na mwenyeji wake, Rais Samia yatakayofuatiwa na mazungumzo rasmi ya kujadili namna ya kukuza ushirikiano baina ya nchi hizi mbili.
Kadhalika viongozi hao kwa pamoja watazungumza na waandishi wa habari kuelezea makubaliano waliyofikia katika mazungumzo yao, kabla ya kushiriki dhifa ya chakula cha jioni iliyoandaliwa na Rais Samia kwa heshima ya Dk Nandi-Ndaitwah.

Akiendelea na ziara yake nchini, Nandi-Ndaitwah, Mei 21, 2025 anatarajiwa kutoa Mhadhara katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam pamoja na kutembelea Kituo cha Urithi wa Ukombozi wa Afrika kilichopo Dar es Salaam.
Tanzania na Namibia zimeendelea kuimarisha ushirikiano wa kihistoria ulioasisiwa na waasisi wa mataifa hayo mawili hayati Mwalimu Julius Nyerere na hayati Sam Nujoma, kupitia mikataba mbalimbali ya uwili na masuala yote yanayohusu Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).