Rais wa Misri kushuhudia uzinduzi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere

Dar es Salaam. Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri, Dk Badr Abdelatty amesema Rais wa nchi hiyo Abdel Fattah al Sisi anashauku kushuhudia uzinduzi wa mradi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere (JNHPP), ambalo ujenzi wake umefikia asilimia 99.9.

Dk Abdelatty ambaye yupo nchini kwa ziara ya kikazi, jana Jumatano Machi 19, 2025 amesema kuwa atafanya mazungumzo na Rais Samia Suluhu Hassan kupanga siku ya uzinduzi ili kiongozi wa Taifa hilo ashiriki.

Mbali na hilo, Dk Abdelatty ameainisha maeneo  ambayo nchi hiyo ipo tayari kushirikiana na Tanzania katika kukuza uchumi wenye manufaa kwa pande zote hasa katika kilimo, teknolojia, elimu, nishati ya maji, miundombinu   na biashara.

Mradi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere (JNHPP) unatekelezwa na muungano wa Misri unaojumuisha Kampuni za Al-Maqawon Al-Arab na Al-Suwaidi.

Mradi huo unaojengwa kwa gharama ya Sh6.6 trilioni, mpaka kukamilika kwake, utazalisha megawati 2,115 za umeme.

Aidha, Dk Abdelatty ameambatana na wafanyabiashara 12 ambao wapo nchini wakifanya mazungumzo na wafanyabiashara 25 wa Tanzania pamoja na sekta zinazohusika na uwekezaji, lengo kuangalia fursa zilizopo na kuzichangamkia.

Akizungumzia Bwawa la Nyerere, Dk Abdelatty amesema bwawa hilo ujenzi wake umefikia asilimia 99.9 na akisisitiza uwepo wa bwawa hilo ni nguzo muhimu kuonyesha ushirikiano baina ya Tanzania na  Misri.

“Bwawa hili ni mfano bora wa ushirikiano wa Afrika katika miradi ya umeme wa maji, na Misri imejitolea kikamilifu kuhakikisha mradi huu unakamilika,” amesema.

Amesema mradi wa umeme wa maji utaifanya Tanzania kuwa na umeme wa uhakika jambo ambalo litachochea ukuaji wa viwanda pamoja na maendeleo nchini akisisitiza wataalamu wa Taifa hilo wamefanya juu chini kuhakikisha mradi huo unakamilika.

Dk Abdelatty amesema nchi ya Misri inapanua uwekezaji wake kwa nchi za mto Nile pamoja na kukuza uchumi wa Tanzania ambapo sasa wameanzisha Mfuko wa Uwekezaji kwa lengo la kuboresha miundombinu na miradi ya nishati itokanayo na maji.

“Nchi ya Misri ndio mfadhili mkubwa wa miradi ya maendeleo kwa nchi zinazopitiwa na Mto Nile na tumekuwa tukifuata sheria  na kuhakikisha pande zote zinapata manufaa,” amesema.

Katika eneo la biashara amesema Misri inafanya vyema katika eneo la dawa hivyo ushirikiano baina ya Tanzania na nchi hiyo sio tu utaifanya Tanzania kuwa soko bali eneo watakalotengeneza viwanda vitakavyochochea ajira ya watu nchini.

Amesema biashara baina ya mataifa hayo inakua lakini yapo maeneo ambayo bado fursa hazija changamkiwa.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo amesema ziara ya kiongozi huyo ni kufanya maandalizi ya ufunguzi wa Bwawa la Nyerere ambapo atakutana na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko na Rais Samia kupanga ufunguzi wa bwawa hilo.

“Lengo la ziara yake ni kufanya maandalizi ya ufunguzi wa bwawa la Mwalimu Nyerere na atakutaka na Rais Samia Suluhu Hassan kupanga mazungumzo ya mwisho ya ufunguzi wa bwawa hilo,”

Maeneo ya ushirikiano

Mbali na kuzungumzia mradi huo wa maji wa Julias Nyerere, Balozi Kombo amesema Serikali ya Misri imeridhia kuongeza ushirikiano na Tanzania katika sekta ya elimu, afya, kilimo, biashara na maji hususan upande wa maziwa yaliyopo nchini na miundombinu.

“Eneo lingine ni uhifadhi wa mazao  ya Kilimo kuepuka upotevu na  yakae kwa  muda mrefu na kusafirishwa nje ya nchi, pia wamekubali vijana wetu kwenda kusoma Misri wakitupa uwanja mpana  tupeleke idadi yeyote,” amesema.

“Vijana 60 kwa mwaka ndio walikuwa wanaenda kusoma nchini Misri lakini sasa fursa hiyo imeongezeka na watakwenda kusoma fani ya udaktari, uvuvi, sayansi na uhandisi viwandani,” amesema.

Kwa eneo la biashara amesema kati ya wafanyabiashara 12 waliokuja nchini kutokea Misri wawili wameonyesha nia ya kuweka kwenye kilimo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *