Rais wa Iran: Moto wa vita wa Wazayuni ukomeshwe kwa kuwashinikiza wanaowaunga mkono

Rais wa Iran ametaka kushinikizwa waungaji mkono wa utawala wa Kizayuni ili kusitisha moto wa vita na jinai za mauaji ya kimbari zinazotekelezwa na utawala huo.

Rais Masoud Pezeshkian jana alizungumza kwa simu na Haitham bin Tariq Sultan wa Oman na kupongeza misimamo thabiti ya Oman dhidi ya jinai za utawala wa Kizayuni huko Gaza na Lebanon. Pezeshkian aidha amesisitiza kushinikizwa waungaji mkono wa utawala wa Kizayuni ili kukomesha moto wa mauaji na jinai za utawala huo ghasibu.  

Jinai na mauaji ya kimbari ya Israel dhidi ya wakazi wa Ukanda wa Gaza 

Rais Masoud Pezeshkian ametaja kuimarisha uhusiano kati ya Iran na Oman kuwa kati ya vipaumbele vya sera kuu za Jamhuri ya Kislamu katika kustawisha uhusiano na majirani zake na kuongeza kuwa kuimarisha uhusiano wa kirafiki na wa karibu kati ya nchi za eneo hili pamoja na kupanua ushirikiano wa kikanda ni dhamana ya kuwa na mtazamo na lugha ya pamoja kwa ajili ya kutatua matatizo na changamoto mbalimbali za kikanda kama jukwaa la maendeleo ya pamoja ya nchi na kukuza ustawi, amani na utulivu wa watu wetu.”

Katika mazungumzo hayo ya simu, Sultan wa Oman amesema kuwa kuunga mkono haki za wananchi madhulumu wa Gaza na Lebanon ni katika vipaumbele na daghadagha kuu za nchi yake na kwamba Oman siku zote inasisitiza kuwa uungaji mkono endelevu wa nchi za Magharibi kwa jinai za Israel haukubaliki na hauwezi kuhalalishwa kwa namna yoyote ile.