Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, anasema ana imani kwamba mkutanowa dharura wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu utatoa matokeo “yakinifu na yanayoonekana” katika kusimamisha ukatili wa utawala wa Israel huko Gaza na Lebanon.
Pezeshkian ameyasema hayo katika mazungumzo ya simu na Mwanamfalme wa Saudia, Mohammed bin Salman, jana Jumapili wakati Riyadh ikitarajiwa kuwa mwenyeji wa viongozi wa nchi za Kiarabu na za Kiislamu kwa ajili ya mkutano uliopangwa kufanyika leo Jumatatu utakaoangazia vita vya Israel huko Gaza na Lebanon.
Mkutano wa kilele wa OIC na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu umepangwa kujadili vita vya mauaji ya halaiki ya Israel huko Gaza na uchokozi wake dhidi ya Lebanon pamoja na matukio ya sasa katika eneo la Magharibi mwa Asia.
“Sina shaka kwamba mkutano huu wa kilele utakuwa na matokeo madhubuti na yanayoonekana yatakayopelekea kusitishwa jinai za utawala wa Kizayuni na vita na umwagaji damu huko Gaza na Lebanon,” amesema Rais Pezeshkian.

Ameongeza kuwa hakuweza kukubali mwaliko wa Mfalme wa Saudia kushiriki katika mkutano huo kutokana na kazi nyingi ya kiutendaji, lakini amesema kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais, Mohammad Reza Aref atashiriki katika mkutano huo.
Rais wa Iran ameeleza matumaini yake kuwa Tehran na Riyadh zitaboresha zaidi uhusiano katika nyanja zote kwa kuzingatia azma ya pande zote mbili.
Kwa upande wake, Mwanamfalme wa Saudia amepongeza mabadiliko ya kihistoria katika uhusiano wa Tehran na Riyadh na kueleza matumaini yake kuwa uhusiano wa pande zote mbili utafikia viwango vya juu katika nyanja zote.
Salman ameongeza kuwa atatumia fursa ya kuwepo Makamu wa Rais wa Iran mjini Riyadh kujadili njia za kupanua uhusiano wa pande mbili.
Kwa mara nyingine tena amemwalika Rais wa Iran kwenda Saudi Arabia na kueleza matumaini kwamba kutatayarishwa uwanja wa suala hilo haraka iwezekanavyo.