Rais wa Iran atoa wito kwa Papa Francis kusaidia kukomesha jinai za Wazayuni huko Gaza, Lebanon

Rais wa Iran Masoud Pezeshkian, katika ujumbe wake kwa Papa Francis, ametoa wito wa kumtaka atumie ofisi yake kusaidia kukomesha “uvamizi usio wa kibinadamu” wa utawala wa Israel dhidi ya watu wa Gaza na Lebanon, na kuanzisha usitishaji vita ili kuzuia kuenea kwa vita katika eneo la Asia Magharibi.

Ujumbe wa Rais Pezeshkian uliwasilishwa kwa mkuu wa Kanisa Katoliki siku ya Jumatano na Mohammad Mehdi Imanipour, Mkuu wa Shirika la Utamaduni na Mahusiano ya Kiislamu la Iran (ICRO). Imanipour anaongoza ujumbe wa Iran unaoshiriki katika toleo la 12 la mazungumzo ya dini mbalimbali kati ya Iran na Vatican, ambayo yamefanyika nchini Italia kuanzia 19-20 Novemba.

Rais wa Iran katika ujumbe wake ameashiria zaidi ya mwaka mmoja wa mashambulizi ya kikatili ya utawala wa Israel huko Gaza na hivi sasa huko Lebanon na kusema kuwa, mashambulizi hayo ya kinyama yanaendelea kwa kiasi kikubwa bila kuzingatia sheria na kanuni za kimataifa.

Rais wa Iran amesema katika ujumbe wake kwambe: “Mauaji ya halaiki na uharibifu mkubwa wa miundombinu ya mijini na afya unafanyika wakati ambao wengi wa mashahidi na waliojeruhiwa ni watoto na wanawake.”

Pezeshkian amebainisha masikitiko yake kwamba ukiukwaji huu wa haki za binadamu unafanywa katika ardhi takatifu ambayo ni mahali pa kuzaliwa manabii na wajumbe wa amani na utulivu kwa wanadamu.

Amesema kwa kutilia maanani nukta hizo na kuwepo vitisho kwa amani na usalama wa kieneo na kimataifa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa ikifanya juhudi maalumu za kukomesha mauaji na kujeruhiwa zaidi watu wasio na hatia kwa kuanzisha usitishaji vita na kuzuia kuenea vita.

Pezeshkian ameashiria mauaji yaliyotekelezwa na Israel dhidia kiongozi wa kisiasa wa Hamas Ismail Haniyeh jijini Tehran mwishoni mwa Julai, ambayo yalitekelezwa saa chache baada ya kuapishwa kwake kama rais wa Iran.

Amesema Iran ilikusudia kutoa jibu la haraka kwa Israel, kwa kuzingatia kanuni za Mkataba wa Umoja wa Mataifa za ulinzi halali wa ardhi yake.

Hata hivyo, ameongeza kuwa, Iran ilichelewesha majibu yake kufuatia jumbe za viongozi wa nchi za Magharibi kwamba mapigano yatasitishwa Gaza.

Amesema licha ya Iran kujizuia kuchukua hatua haraka, utawala wa Israel uliendelea na uchokozi wake na kufanya mashambulizi makubwa dhidi ya Lebanon, ambayo bado yanaendelea hadi sasa.

Amesema: “Katika hali hii ya taharuki na uwezekano wa kuenea vita katika eneo hili, nakuomba kwa heshima wewe Mkuu wa Kanisa Katoliki, utumie ofisi zako nzuri kuzuia kuendelea kwa fujo zisizo za kibinadamu, kuweka amani na usitishaji vita na kuunda fursa ya kuwasilisha misaada ya kibinadamu kwa waathirika.”

Rais Pezeshkian pia ametoa wito kwa Papa Francis kuwahimiza viongozi wa dunia, hasa nchi za Kikristo, kusaidia katika juhudi hizo muhimu za amani.

Rais wa Iran amesema, hatua hiyo bila shaka itakuwa na taathira kubwa katika kupunguza mateso ya wahanga na kushughulikia mahitaji ya watu wasiojiweza na kusisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iko tayari kusaidia katika mchakato huo.