Rais wa Iran amehudhuria hafla ya mazishi ya jenerali aliyeuawa shahidi Abbas Nilforoushan, mshauri wa ngazi za juu wa kijeshi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Lebanon.
Kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA, rais Masoud Pezeshkian wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema katika hafla ya mazishi ya Shahidi Nilforoushan, kwamba taifa la Iran litasimama kidete hadi mwisho.
Brigedia Jenerali Ismail Qaani, kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC), pamoja na maafisa wa kijeshi na kitaifa wamehudhuria hafla za kuukaribisha mwili wa Shahidi Jenerali Abbas Nilforoushan mjini Tehran leo asubuhi Jumanne.
Mohammad Bagher Ghalibaf Spika wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa katika mahojiano na kanali ya televisheni ya “Al-Mayadeen” kuhusu uvumi kuhusiana na Jenerali Qaani kwamba: “Uvumi unaoenea kuhusu Jenerali Qaani ni katika hali ya kueneza habari za uwongo na zenye uzushi.”

Hafla za kumuaga Jenerali Nilforoushan zitafanyika kesho (Jumatano) huko Isfahan, na hatimaye maziko ya shahidi huyo wa ngazi ya juu pia yatafanyika Alhamisi alasiri huko Isfahan, katikati mwa Iran.
Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala ghasibu wa Kizayuni, alitoa amri ya kuuawa Sayyid Hassan Nasrullah, Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon, siku ya Ijumaa ya tarehe 27 Septemba akiwa katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, kwa uungaji mkono wa Marekani.
Kutokana na amri hiyo, ndege za kivita za utawala katili wa Kizayuni zilishambulia kwa mashambulizi makali dhidi ya maeneo ya makazi ya raia huko “Hareh Harik” kusini mwa Beirut kwa mabomu ya pauni 2,000 ambapo wapigana jihadi akiwemo Sayyid Hassan Nasrullah na Jeneralo Nilforoushan waliuawa shahidi.