Rais wa Finland kufanya ziara ya siku tatu Tanzania

Dar es Salaam. Rais wa Finland, Alerander Stubb anatarajia kufanya ziara ya Kitaifa ya siku tatu kuanzia kesho Jumatano, Mei 14, 2025 nchini Tanzania.

Baada ya kuwasili, Stubb atapokewa na mwenyeji wake, Rais Samia Suluhu Hassan katika Ikulu ya Magogoni jijini Dar es Salaam.

Taarifa iliyotolewa leo Jumanne, Mei 13, 2025 na Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Shaaban Kissu imesema kiongozi huyo atafanya ziara ya kitaifa kwa mwaliko wa Rais Samia.

“Katika ziara hiyo, Rais Stubb atashiriki matukio mbalimbali ikiwemo semina kuhusu Urithi wa hayati Mariti Ahtisaari, Rais mstaafu wa Finland na mwanadiplomasia mbobezi aliyeshika nafasi mbalimbali ikiwemo Mjumbe Maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Namibia na Kosovo, pia aliwahi kuwa Balozi wa Finland nchini Tanzania,” amesema Kissu.

Amesema mbali na viongozi wa kiserikali, Rais Stubb ataambatana pia na wafanyabiashara kutoka nchini Finland.

“Atahutubia katika jukwaa la wafanyabiashara wa Tanzania na Finland linalotarajiwa kufanyika Mei 16, 2025, litakalojadili fursa za kiuchumi na biashara baina ya nchi hizi mbili,” amesema.

Amesema jukwaa la wafanyabiashara litakuwa chachu ya kuchochea biashara na uwekezaji baina ya nchi hizo mbili, Tanzania ikitegemea kunufaika na mitaji na uwekezaji kutoka Finland.

Kissu amesema Rais Stubb atahutubia katika semina ya vijana kuhusu masuala ya uvumbuzi itakayofanyika Kituo cha Mikutano cha Julius cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) iliyoandaliwa na Shirika la Kimataifa la Maendeleo (UNDP).

Pia, anatarajia kuzindua mradi wa Pandamiti Kibiashara (FORLAND) katika bustani ya Jiji (Botanical Gardens) pamoja na kutembelea Mradi wa Wanawake Wanaweza, unaoratibiwa na UN Women uliopo Machinga Complex Ilala.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *