Rais Joao Lourenco wa Angola ametoa mwito wa kukomeshwa jinai za utawala wa Kizayuni huko Lebanon na Palestina na kusisitizia haja ya kuundwa taifa huru la Palestina.
Rais Lourenco amesema hayo wakati alipotoa hotuba yake ya kila mwaka kuhusu hali ya taifa mbele ya Bunge la nchi hiyo mjini Luanda na kusisitiza kwa kusema: “Ulimwengu hauwezi kuendelea kushuhudia raia na watu wasio na hatia wakiuawa kila siku tena kwa sura ya kutisha huko Ghaza, Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Lebanon.
Vile vile amesema: “Angola inaunga mkono juhudi za kutafuta amani ya kudumu katika eneo hilo, chini ya msingi wa kuheshimiwa Mkataba wa Umoja wa Mataifa, sheria ya kimataifa inayopiga marufuku kuvamiwa maeneo ya mataifa mengine sambamba na kuheshimiwa mipaka na uhuru wa nchi nyingine.”

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake kwenye Bunge, Rais wa Angola amesema, kuna wajibu wa kukomeshwa kukaliwa kwa mabavu ardhi za nchi nyingine, kuundwa na kutambuliwa rasmi nchi huru ya Palestina katika mipaka ya mwaka 1967 na kutolewa walowezi wa Kizayuni katika maeneo ya Wapalestina wanayoyakalia kwa mabavu.
Rais Lourenco amesema: “Jamii ya kimataifa lazima iungane, ishikamane na ifanya jitihada za pamoja za kukomesha vita hivi, kulinda maisha ya watu wasio na hatia huko Ghaza, Ukingo wa Magharibi na Lebanon na kudumisha amani na usalama katika eneo la Mashariki ya Kati (Asia Magharibi) hasa kwa kuzingatia kuwa migogoro ya eneo hili ina taathira kubwa hasi kimataifa.