Angola. Unaweza kuiita ziara ya kihistoria kwa Rais Samia Suluhu Hassan aliyoifanya nchini Angola kwa mara ya kwanza tangu aingie madarakani Machi 19, 2021.
Rais Samia alikuwa nchini humo kwa ziara ya siku tatu aliyoianza Aprili 7, 2025 na kuihitimisha jana baada ya kupokea mwaliko kutoka kwa Rais wa Angola, João Lourenço.
Mbali ya kazi zingine alizozifanya katika ziara hiyo, Rais Samia pia amejiwekea historia ya kuwa Rais wa kwanza mwanamke kulihutubia bunge la nchi hiyo.
Licha ya baadhi ya nchi barani Afrika kuwa na marais kadhaa wanawake, lakini Rais Samia ndiye aliyepatiwa fursa ya mwaliko wa Rais wa Bunge la Angola, Caroline Carqueira.
Akilihutubia bunge hilo juzi, Rais Samia alisema Bara la Afrika linahitaji mshikamano ili liweze kuwa imara na kuheshimika.
“Giza linaloonekana katika bara letu ni kielelezo kuwa, tunahitaji kuwa na mshikamano utakaozifanya nchi zetu kuwa imara,” alisema Rais.
Alisema mshikamano utakaooneshwa na nchi za bara hilo, sio tu kupambana na umaskini, bali pia utalifanya Bara la Afrika kuheshimika.
Alisema kwa kushirikiana na Rais mwenzake wa Angola, wamekubaliana kushirikiana na kuhakikisha changamoto zinazozikumba nchi hizo mbili zikiwamo za kuimarisha uchumi wanapambana nazo ili kuleta maendeleo si ya nchi hizo tu bali kwa bara zima la Afrika.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akiangalia historia ya Kiwanda cha kusafisha Mafuta cha Luanda Oil Refinery wakati akihitimisha ziara yake Jijini Luanda nchini Angola tarehe 09 Aprili, 2025.
Alimpongeza Rais Lourenco kwa kuimarisha uchumi wa nchi yake na kupambana na rushwa na kuwataka wananchi wa nchi hiyo kuendelea kumuunga mkono rais wao katika mapambano hayo.
Aidha, Rais Samia alitangaza msamaha wa viza ya kitalii kwa raia wa Angola wanaotaka kutembelea nchini.
Hatua hiyo yanatajwa kuwa itaongeza tija katika sekta ya usafiri, uwekezaji na biashara kati ya mataifa hayo mawili.
“Nina furaha kutangaza juu ya msamaha wa viza ya kitalii kwa raia wa Angola wanaotaka kutembelea Tanzania,” alisema.
Hata hivyo, Rais Lourenco alisema uchumi wa Angola hivi sasa unafikia Dola 100 bilioni za Marekani (Sh266.6 trilioni) umelifanya Taifa hilo kuwa na uchumi imara unaotokana na biashara ya mafuta na madini.
Ziara ya Rais Samia Angola ni ya kuimairisha uhusiano wa nchi hizo mbili uliojengwa na waasisi hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na hayati Agustino Neto wakati wa harakati za ukumbozi wa nchi ya Angola.
Rais Samia alitembelea nchi hiyo baada ya kupita miaka 19 tangu Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete alipotembelea nchi hiyo mara ya mwisho mwaka 1996.
Rais Samia alisema Tanzania ina fursa nyingi za uwekezaji na amewakaribisha wananchi wa Angola kuitembelea na Watanzania kutafuta fursa nchini humo.
Alisema Tanzania ina hazina kubwa ya gesi na madini ambayo bado haijatumika vya kutosha.
“Nikupongeza Spika wa Bunge, Caroline kwa kuwa mfano mzuri wa kuliendesha Bunge hili kidemokrasia, huu ni mfano wa kuigwa,” alisema Rais Samis.

Aliahidi kuwa katika ziara yake ambayo ameambatana na baadhi ya wabunge, itaendeleza uhusiano wao wa kutembeleana na anawaruhusu kufanya hivyo.
Aidha, alisema Tanzania kihistoria ilisimama imara kuisaidia Angola kwa juhudi zake za kupambana na utawala wa kikoloni ndio maana, baadhi ya maeneo yamepewa majina ya wapigania uhuru wake.
Rais Samia alisema nchi za Afrika bado zinachangamoto ya ulinzi na usalama ndiyo maana katika hati za makubaliano walizotiliana saini jana, suala la usalama limepewa kipaumbele.
Licha ya kulihutubia Bunge, Rais Samia pia alishudia Tanzania na Angola zikitiliana saini mikataba miwili yenye lengo la kuimarisha uhusiano baina ya nchi mbili hizo.
Miongoni mwa mikataba hiyo ni pamoja na wa Rasimu ya Mkataba wa Ushirikiano katika Sekta ya Ulinzi.
Akizungumza na waandishi wa habari Ikulu jijini Luanda, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa wa Tanzania, Dk Stergomena Tax alisema mkataba huo unalenga kuimarisha ulinzi na usalama wa pande zote mbili.
“Pia, unalenga kushirikiana katika sekta ya afya, michezo, utamaduni na jamii na katika maeneo mengine yenye masilahi kwa pande zote mbili,” alisema waziri huyo.
Waziri Tax alisema mkataba huo utadumu kwa miaka mitano na baada ya kuisha muda wake, pande zote zitaanza mazungumzo mengine kwa ajili ya kuhuisha mkataba huo pamoja na kuongeza maeneo mengine ya kushirikiana ikiwa yatajitokeza.
Tanzania pia, imesaini Rasimu ya Hati ya Makubaliano (MOU) Kati ya Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na Wakala wa Uwekezaji Binafsi Ukuzaji na Uwezesha Usafirisha Nje Angola (Apex).
Hati hiyo ya makubaliano inalenga kukuza uwekezaji wa ndani na wa kigeni Tanzania na Angola.
Akizungumza baada ya kusaini makubaliano hayo, Mtendaji Mkuu wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Gilead Teri alisema mkataba huo unalenga pia kuanzisha ushirikiano wa kimkakati baina ya Tanzania na Angola kwa lengo la kukuza uwekezaji wenye masilahi ya kiuchumi kwa nchi zote mbili.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akiagana na Rais wa Jamhuri ya Angola João Manuel Gonçalves Lourenço wakati akihitimisha ziara yake ya kiserikali, Luanda nchini Angola tarehe 09 Aprili, 2025.
“Tunalenga kuzingatia miongozo na kanuni za usawa, ushiriki wa hiari, uaminifu na manufaa ya pamoja kama kuanzisha ushirikiano wa pamoja na kwa faida kati ya taasisi hizi mbili,” alisema Teri.
Alisema lengo lingine ni kukuza ushirikiano wa kidiplomasia kwa lengo la kuendelea kuvutia uwekezaji na wawekezaji sambamba na kukuza biashara ya mauzo ya nje na kuimarisha uhusiano wa kiuchumi na kiteknolojia.
Alisema kuanzishwa kwa mfumo wa ushirikiano wa kukuza uwekezaji wa pamoja, makubaliano hayo yatakuwa ya miaka mitano.
Katika ziara hiyo, Rais Samia aliweka pia shada la maua katika kaburi la muasisi wa Taifa la Angola, Antonio Neto.
Umuhimu wa ziara
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Kombo akizungumzia ziara hiyo, alisisitiza umuhimu wa Tanzania kuangazia maeneo yenye tija kwa maendeleo ya Tanzania na Angola, huku akibainisha ushirikiano wa kweli lazima ujikite kwenye maeneo yenye fursa halisi za kiuchumi, kijamii na kidiplomasia.
Waziri Kombo alisema ziara hiyo ililenga kufungua ukurasa mpya wa ushirikiano wa kimaendeleo kati ya mataifa hayo mawili.
“Ni wajibu wetu kuhakikisha maeneo tutakayojadili katika ziara hii yanaakisi malengo ya kimaendeleo ya nchi zetu. Tuangalie maeneo yenye tija ya moja kwa moja kwa wananchi wetu,” alisema Kombo.
Pia, aliwahimiza wajumbe kutoka taasisi na wizara mbalimbali za Tanzania kutumia fursa ya ziara hiyo, kuchambua kwa kina maeneo yatakayochangia kukuza uchumi, kuongeza ajira na kuinua maisha ya wananchi kupitia ushirikiano wa kimkakati.
Alisema ushirikiano kati ya Tanzania na Angola unapaswa kuimarishwa zaidi katika sekta muhimu kama biashara na uwekezaji, uchumi wa buluu, mafuta na gesi, madini, afya, elimu, miundombinu, utalii, mawasiliano, pamoja na masuala ya ulinzi na usalama wa kikanda.

“Ziara hii ya kihistoria ya Rais Samia inatarajiwa kuleta matokeo makubwa, siyo tu kwa upande wa uhusiano wa kidiplomasia, bali pia katika kutafsiri kwa vitendo fursa zilizopo kwa manufaa ya wananchi wetu,” aliongeza Waziri Kombo.
Alisisitiza kuwa, Tanzania ina nia ya dhati ya kushirikiana na Angola katika miradi ya maendeleo itakayochochea ukuaji wa sekta za kimkakati, kuboresha mifumo ya uchumi na kuimarisha urafiki wa muda mrefu kati ya mataifa hayo mawili.