Rais Samia na miaka minne ya uboreshaji wa miundombinu ya barabara na madaraja

Ilianza kama ndoto, baadaye ukawa uhalisia, ndivyo unavyoweza kuitafsiri miaka minne ya utendaji wa Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, katika sekta ya miundombinu ya barabara na madaraja.

Safari yake ya utendaji katika wadhifa wa urais, ilianza na mashaka kutoka kwa baadhi ya wananchi, wakidhani uendelezaji wa miradi iliyoachwa na mtangulizi wake, kisingekuwa kipaumbele chake.

Hali imekuwa tofauti na wale waliodhani angeshindwa wameshangazwa kutokana na kasi kubwa ambayo Rais Samia anaitumia katika utekelezaji wa miradi hiyo. Serikali ya awamu ya sita kwa kushirikiana na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) imefanya kazi kubwa katika kuhakikisha nchi inakuwa na miundombinu bora ya usafirishjaji.

Barabara na madaraja

Mkurugenzi wa Mipango ya Miundombinu TANROADS, Mhandisi Ephatar Mlavi anasema katika kipindi hicho, barabara zenye urefu wa jumla ya kilometa 15,625.55 zimekuwa katika hatua mabalimbali za utekelezaji ambapo barabara zenye urefu wa jumla ya kilometa 1,365.87 zimekamilika kujengwa kwa kiwango cha lami na barabara zenye urefu wa jumla ya kilometa 2,031.11 zimeendelea kujengwa kwa kiwango cha lami.

Barabara ya Mbinga-Mbamba Bay km 66 iliyokamilika kujengwa kwa kiwango cha lami na kuzinduliwa rasmi Septemba 25, 2024 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan imekuwa kiungo muhimu cha uchumi katika Ukanda wa Kusini.

Barabara zenye urefu wa jumla ya kilometa 2,052.94 na madaraja mawili zime-fanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina na Serikali inatafuta fedha za kuzijenga kwa kiwango cha lami.

Aidha, upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara zenye jumla ya kilometa 4,734.43 na madaraja kumi unaendelea. Miradi ya barabara yenye urefu wa takriban kilometa 5,326.90 na miradi saba ya madaraja ipo katika hatua ya manunuzi kwa ajili ya kufanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ikiwa ni maandalizi kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa barabara hizo kwa kiwango cha lami.

Kukamilika kwa awamu ya pili ya mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) yenye urefu wa kilometa 20.3, inayojumuisha barabara za Mbagala – Mzunguko wa Bandari (Bendera Tatu), Bendera Tatu–Kariakoo, Sokoine – Zanaki na Kawawa–Morogoro (Magomeni).

Pia, utekelezaji wa awamu ya tatu ya mradi huo kutoka katikati ya jiji hadi Gongo la Mboto (km 23.3) umefikia asilimia 74. Aidha, TANROADS inaendelea na ujenzi wa barabara ya mzunguko wa nje wa Dodoma (Outer Ring Road) yenye urefu wa kilometa 112, inayolenga kupunguza msongamano wa magari katikati ya jiji.

Hadi Februari 2025, sehemu ya kwanza ya barabara hiyo (km 52.3) imekamilika kwa asilimia 91, huku sehemu ya pili (km 62) ikiwa imefikia asilimia 85.

Pia, TANROADS inatekeleza miradi inayofadhiliwa na Benki ya Dunia, ikiwemo upanuzi wa barabara zinazoingia na kutoka Dodoma, kama vile barabara ya Chamwino (km 32), Mkonze (km 4.5), na Zamahero (km 8.5), kupitia mradi wa Dodoma Integrated and Sustainable Transport (DIST).

Katika Jiji la Mbeya, barabara kuu ya TANZAM (Uyole–Ifisi–Songwe Air-port) yenye urefu wa kilomita 36 inaendelea kupanuliwa kutoka njia mbili hadi nne ili kupunguza msongamano, ambapo utekelezaji umefikia asilimia 22.

Waziri wa Ujenzi, Mhe. Abdallah Ulega.

Vilevile, upanuzi wa barabara ya Mwanza–Usagara–JPM Bridge (km 37) unaendelea ili kuboresha mtandao wa usafiri mkoani humo. Katika kipindi tajwa madaraja makubwa tisa yamekamilika kujengwa kwa gharama ya Sh 381.301 bilioni ambapo aliyataja madaraja hayo kuwa ni Gerezani (Dsm) na Daraja jipya la Tanzanite (DSM).

Mengine ni Wami (Pwani), Kitengule (Kagera), Kiyegeya (Morogoro), Ruaha (Morogoro), Ruhuhu (Ruvuma), Mpwapwa (Dodoma) na daraja la Msingi (Singida).

Alibainisha kuwa mada-raja 10 ambayo ni Kigongo– Busisi (Magufuli Bridge -Kilometa 3.0), Lower Mpiji (Meta 140), Mbambe (Meta 81), Simiyu (Meta 150), Pangani (Meta 525), Sukuma (Meta 70), Kerema Maziwani (meta 80), Kibakwe (meta 30), Mirumba (Meta 60) na Jangwani (Meta 390) ujenzi wake unaendelea kwa gharama ya Sh 985.802 bilioni.

Madaraja makubwa 19 yako kwenye maandalizi ya kujengwa ambayo ni Godegode (Dodoma), Ugala (Katavi), Kamshango (Kagera), Bujonde (Mbeya), Bulome (Mbeya), Chakwale (Moro-goro), Nguyami (Morogoro), Mkundi (Morogoro), Lower Malagarasi (Kigoma), Mtera (Dodoma), Kyabakoba (Kag-era), Mjonga (Morogoro), Doma (Morogoro), Sanga (Songwe), Kalebe (Kagera), Ipyana (Mbeya), Mkondoa (Morogoro), Kilambo (Mtwara) na Chemchem (Singida).

Katika kipindi hicho hali ya barabara kuu na zile za mikoa imeendelea kuimarika ambapo barabara zilizo katika hali nzuri na wastani zimekuwa karibu asilimia 90 ya jumla ya mtandao wote wa barabara wenye Kilometa 37,225.72.

Hali hii imesababisha kupungua kwa muda wa usafiri katika barabara, kuimarika kwa bei za usafirish-aji ambapo nauli hazipandi kiholela na kuongezeka kwa shughuli za kiuchumi na kijamii zinazotumia barabara.

Udhibiti wa mizigo ya magari

Wizara ya Ujenzi kupitia TANROADS inafanya udhibiti wa uzito wa magari kulingana na Sheria ya Udhibiti Uzito wa Magari ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Mwaka 2016 na Kanuni zake za nwaka 2018 ili zisiharibike mapema na ziweze kudumu kulingana na usanifu wake.

Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Mohamed Besta.

Katika kutekeleza jukumu hilo, mizani zinazohamishika na zisizohamishika hutumika. Idadi ya mizani zisizohamishika imeongezeka kutoka 67 hadi 79 na zinazohamishika kutoka 17 hadi 22 kati ya mwaka 2021/22 hadi Julai 2024.

Katika kupunguza msongamano wa magari katika mizani zenye magari mengi, Wizara ya Ujenzi kupitia TANROADS imefunga mizani ishirini za kupima magari yakiwa kwenye mwendo (Weigh-in-Motion WIM) katika Mikoa ya Pwani, Morogoro, Iringa, Songwe, Dodoma, Singida, Arusha na Mara. Kutokana na udhibiti huo magari yanayozidisha uzito yamepungua kutoka asilimia 0.48 hadi kufikia asilimia 0.26.

Viwanja vya ndege

Kwa upande wa viwanja vya ndege, ujenzi umekamilika kwa miradi saba ya Julius Nyerere (Terminal Three), Mwanza, Mtwara, Songea, Songwe (Runway), Songwe (Supply and Installation of Airfield Ground Lights (AGL) na Geita.

Aidha, kuna miradi minane pia ya viwanja vya ndege ambapo hadi sasa kazi inaendelea, na ipo katika hatua nzuri za ukamilishwaji au maendeleo. Miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa Uwanja wa ndege wa Msala-mkoani Dodoma, Uwanja wa ndege wa Iringa, Uwanja wa ndege wa Musoma na Uwanja wa ndege wa Tabora.

Hatua hizi zinathibitisha msimamo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dk Samia Suluhu Hassan katika kujenga Tanzania ya kisasa, yenye barabara bora, viwanja vya ndege vya kisasa na miundombinu imara kwa maendeleo ya Watanzania wote.

Mkakati wa kupunguza msongamano wa magari Pamoja na Serikali kujenga miundombinu mingi na bora, lakini kutokana na ukuaji wa uchumi kumekuwepo na ongezeko kubwa la magari katika barabara na hivyo kusababisha msongamano wa magari hayo.

Kwa kutambua hilo Serikali imeweka mpango mahususi na kuanza utekelezaji wake, lengo likiwa ni kupunguza msongamano wa magari hasa katika maeneo ya miji mikubwa.

Hatua zilizochukuliwa na zinazoendelea kuchukuliwa ili kukabiliana na hali hiyo ni pamoja na ujenzi wa njia zaidi za mabasi yaendayo haraka katika Jiji la Dar es Salaam, ujenzi wa barabara za juu (flyover) na ujenzi wa barabara za mchepuko. Serikali imechukua hatua nyingine ya upanuzi wa barabara, ili kukabiliana na kasi ya ongezeko la magari.

Kuimarisha ushirikiano wa kikanda kupitia barabara

Juhudi za Serikali ya awamu ya sita katika utekelezaji wa miradi ya miundombinu ya barabara nchini inavuka mipaka, ikiweka nchi kama mhusika muhimu katika juhudi za ushirikiano wa kikanda wa Afrika. Eneo Huru la Biashara Afrika (AfCFTA) linasisitiza uunganishaji na mitandao ya barabara ya Tanzania ni muhimu katika mafanikio yake.

Barabara kuu kama vile Tunduma-Mpika inayounganisha Tanzania na Zambia, inarahisisha usafirishaji wa bidhaa na watu Afrika Mashariki, Kati na Kusini.

Daraja la Ruaha Mkuku lenye urefu wa mita 133 pamoja na barabara ya Kidatu-Ifakara yenye urefu wa km 66.9 zote zimekamilika na kuzinduliwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan Agosti 4, 2024.

Barabara hizi zimepunguza gharama za usafirishaji, kuimarisha biashara na kukuza ushirikiano wa karibu kati ya mataifa ya Afrika. Kwa kufanya kazi kama kitovu cha kikanda, Tanzania inasaidia kuifanya Afrika kuwa bara lenye umoja na ustawi zaidi.

Ushiriki wa wazawa katika utekelezaji wa miradi hali ya ushiriki wa makandarasi, washauri elekezi na wanawake katika utekelezaji wa miradi katika miradi ya matengenezo ni ya kuridhisha.

Hata hivyo, ushiriki wao katika miradi ya ujenzi wa barabara kuu na barabara za mikoa hairidhishi. Idadi ndogo ya wanawake kushiriki kuomba zabuni, Wanawake kusumbuliwa na changamoto za kifamilia zinazowataka muda mwingi kuhudumia familia.

Hata hivyo wanawake wakandarasi wanashauriwa kushiriki kwenye semina zinazoendeshwa Bodi ya Usajili wa Wakandarasi, kuendelea uhamasishaji na semina mbalimbali za kuwawezesha wanawake kushiriki katika kazi za matengenezo ya barabara.

Rais Samia ang’ara tuzo za ujenzi wa miundombinu

Mwaka 2022 Rais Samia Suluhu Hassan alitunukiwa tuzo ya mwaka 2022 ya mjenzi mkuu, Babacar Ndiaye kwa mafanikio ya Serikali ya awamu ya sita katika ujenzi wa miundombinu ya usafirishaji ambayo kwa kawaida hutolewa kwa mkuu wa nchi iliyofanya vizuri katika sekta hiyo.

Tuzo hii imetolewa kwa kutambua mchango wake kama mwanamke mzalendo na Rais wa kwanza wa Tanzania kupata tuzo hiyo akiwa anaongoza Serikali ya awamu ya sita kwa mafanikio makubwa katika kuendeleza sekta ya miundombinu ya usafirishaji hususani eneo la barabara.

Rais Dk Samia amekuwa na mchango mkubwa katika mafanikio ya utekelezaji wa majukumu ya TANROADS katika kipindi cha miaka minne. TANROADS imekuwa na mipango mingi ili kuhakikisha nchi inakuwa na barabara nyingi za lami ikiwemo kushirikiana na sekta binafsi kwa ajili ya kujenga barabara kwa kiwango cha lami jambo ambalo Rais Samia na Serikali wamekuwa wakiliunga mkono kwa vitendo.

Waziri Ulega na mkakati wa kuendeleza kasi ya utekelezaji wa miradi

Tangu kuteuliwa kwake na Rais Samia Suluhu Hassan, Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega ameonyesha juhudi kubwa katika kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya miundombinu.

Kupitia usimamizi wake, miradi mingi inaendelea kutekelezwa kwa ufanisi. Kwa mfano, katika Jiji la Dar es Salaam, miradi mitano kati ya kumi na moja ya miundombinu ya barabara imekamilika, huku mingine sita ikiendelea.

Miradi hii inajumuisha ujenzi wa miundombinu ya Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) awamu ya pili na ya tatu. Aidha, chini ya uongozi wa Waziri Ulega, Serikali imeendelea kutenga fedha kwa ajili ya matengenezo ya barabara, ikijumuisha matengenezo ya muda maalum, matengenezo ya kawaida na matengenezo ya maeneo korofi na madaraja.

Jitihada za Waziri Ulega zimeleta mafanikio makubwa katika kuboresha miundombinu hivyo kuchangia katika ukuaji wa uchumi na ustawi wa wananchi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *