
Angola. Ikiwa leo ni siku ya tatu na ya mwisho ya ziara ya kikazi ya Rais Samia Suluhu Hassan nchini Angola, asubuhi hii atatembelea kiwanda cha kusafisha mafuta (Luanda Oil Refinery).
Historia inaonyesha nchi ya Angola ni ya pili barani Afrika kuwa na hifadhi kubwa ya mafuta na uchumi wake unaendeshwa zaidi kwa bidhaa hiyo. Tanzania ni miongoni mwa nchi zenye hifadhi kubwa ya gesi barani Afrika.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Sharifa Nyanga, ziara ya Rais Samia leo Jumatano Aprili 9, 2025 kiwanda hapo, kunatoa fursa kwa nchi mbili hizi kubadilishana uzoefu katika sekta ya mafuta na gesi pamoja na kujenga uwezo wataalamu wake.
Nyanga amesema akiwa kiwandani hapo, Samia atapokelewa na Waziri wa Madini wa Angola, Diamantino Pedro Azevedo.
Rais Samia yuko nchini humo kwa mwaliko wa Spika wa Bunge la Angola, Carolina Cerqueira ambaye pia ni mwanamke na Samia anakuwa ni Rais wa kwanza Mwanamke kutoka barani Afrika ambaye jana jioni alipata fursa ya kulihutubia Bunge hilo.
Ikumbukwe ziara hiyo inakuja miaka 19 tangu maraisi wa Tanzania kufanya ziara za kiserikali nchini humo ambapo ziara ya kwanza ilifanywa na Baba wa Taifa.
Halafu ikifuatiwa na Rais wa awamu ya nne Jakaya kikwete, mwaka 2006 ambapo pia alihutubia Bunge la nchi hiyo kama Rais wa Tanzania na Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU).