Rais Samia kukabidhi tuzo ‘Samia Kalamu Awards’

Dar es Salaam. Tuzo 31 zinatarajiwa kukabidhiwa kwa waandishi wa habari katika fainali ya Tuzo za ‘Samia Kalamu Awards’, zitakazotolewa Mei 5, 2025 jijini Dar es Salaam.

Katika tuzo hizo zitakazozotelewa na Rais Samia Suluhu Hassan, kutakuwa na tuzo za chombo cha habari, mwandishi mwenye mafanikio, mwandishi mahiri ofisa habari bora na habari kuhusu nishati safi katika vyombo vya magazeti, redio, tv na mitandao ya kijamii.

Hayo yamesemwa leo Jumamosi Mei 3, 2025 na Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Utangazaji kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Jan Kaaya alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu mchakato wa uhakiki na uchambuzi wa kazi hizo kwa waandishi walioshiriki.

Tuzo hizo zimeandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa) kwa ushirikiano na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania ambazo zilizinduliwa rasmi Oktoba 13, 2024 zikiwa zimebeba kaulimbiu ‘Uzalendo Ndiyo Ujanja’.

Kaaya amesema malengo ya utoaji wa tuzo hizo yanalenga kutambua na kuhamasisha waandishi wa habari wa Kitanzania wanaoandika, kutangaza na kuchapisha kazi zenye maudhui ya maendeleo ya kijamii, kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni.

“Lengo ni kuchochea uandishi wa makala zenye kina zenye kuchambua kwa ufasaha masuala ya maendeleo, kuwajibika kwa jamii, kuimarisha uzalendo na kuchangia katika kujenga chapa na taswira chanya ya Taifa,” amesema Kaaya.

Awali jaji kiongozi wa tuzo hizo, Egbert Mkoko, amesema katika mchakato huo, kazi 1,131 ziliwasilishwa kati ya hizo 263 zilikuwa zikitoka kwenye magazeti, 302 (redio), 275 (televisheni) na 291 kutoka kwa waandishi wa mitandao ya kijamii na tovuti.

Dk Mkoko amesema vigezo vilivyozingatiwa katika utoaji wa tuzo hizo ni pamoja na ulinganifu wa kazi na mada ya maendeleo, ubora wa uandishi na matumizi ya lugha.

Jingine ni utafiti na uchambuzi wa kina, ushawishi wa matokeo, uzingatiaji maadili ya taaluma, mapokezi ya hadhira na matokeo chanya.

Kuhusu changamoto walizokutana nazo katika kuzichambua kazi hizo, mmoja wa majaji, Penzi Nyamungumi amesema kazi nyingi hazikuwa na sauti za wananchi na badala yake viongozi ndio walipewa nafasi zaidi ya kusikika.

Jingine Penzi amesema ni matumizi yasiyo sahihi ya lugha ya Kiswahili, kutolinda utu wa mtu na habari nyingi kutegemea matukio badala ya mwandishi kuzichimba na kuzifanyia kazi mwenyewe.

“Pamoja na changamoto hizo matarajio yetu baada ya tuzo hizi ni kuleta chachu katika kuwahabarisha wananchi na kuwa na habari nyingi za kimaendeleo,” amesema jaji huyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *