Rais Samia kugharimia ukarabati msikiti Milo

Pwani. Baada ya kusambaa kwa kipande cha video kinachoonyesha hali mbaya ya Msikiti wa Milo, mkoani Pwani, Rais Samia Suluhu Hassan ameelekeza ukarabatiwe haraka.

Akizungumza baada ya kufika katika msikiti huo jana Jumanne, Februari 18, 2025,  Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Waleed Omar amesema tayari ameshazungumza na waumini wa msikiti huo kujua changamoto na mahitaji.

Amesema baada ya hatua hiyo, ukarabati wa msikiti utaanza mara moja kama ambavyo Rais Samia ameagiza ili waumini wapate maeneo mazuri ya kufanya ibada.

“Rais Samia aliona picha jongefu mbalimbali za msikiti huu na ameona kuna haja ya kujenga. Na ameguswa amenituma nije kuangalia kwa macho ili afanikishe ujenzi,” amesema.

Amesema Rais Samia mwenyewe ndiye atakayesimamia ujenzi huo hadi pale utakapokamilika, zaidi angependa aendelee kuombewa dua kufanikisha kazi hiyo.

Sheikh Waleed amesema baada ya safari hiyo atakwenda tena kwa ajili ya kuanza rasmi shughuli za ujenzi wa msikiti huo kwa viwango vitakavyostahili.