
Dar es Salaam. Ikiwa zimebaki siku mbili kabla ya kuanza kwa mkutano wa 11 wa mafuta na gesi wa Afrika Mashariki (EAPCE’25), utakaofanyika jijini Dar es Salaam Machi 5, 2025, sekta ya nishati katika kanda ya Afrika Mashariki inajiandaa kwa mijadala itakayochangia mwelekeo wa baadaye wa nishati hizo.
Mkutano huo unatarajiwa kuwa miongoni mwa mikutano yenye ushawishi mkubwa zaidi katika historia ya sekta ya mafuta na gesi, na utafunguliwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
Inaelezwa kuwa zaidi ya washiriki 1,000 wanatarajiwa kushiriki, na Tanzania itatangaza mzunguko wa tano wa utoaji wa leseni za utafutaji wa mafuta na gesi, ikilenga kuvutia wawekezaji katika maeneo ya Mnazi Bay North, West Songo Songo, na Eyasi Wembere.
Akizungumzia mkutano huo leo Jumapili, Machi 2, 2025 Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Felchesmi Mramba, amesema mbali ya Tanzania, Kenya kwa upande wake inalenga kuvutia wawekezaji wapya kwa kuendeleza miradi ya mafuta katika Bonde la South Lokichar, huku Rwanda ikijiandaa rasmi kuingia kwenye sekta ya mafuta na gesi kwa mara ya kwanza.
“Hatua hizi zinatarajiwa kuongeza mvuto wa uwekezaji na kuchochea uzalishaji wa nishati katika kanda,” amesema Mramba.
Amesema gesi asilia inaendelea kuwa mhimili wa maendeleo ya nishati Afrika Mashariki, huku mataifa yakiongeza uwekezaji katika upanuzi wa miundombinu, matumizi ya ndani, na biashara ya gesi.
Mramba amesema tayari Tanzania imeonyesha jinsi gesi inavyoweza kuwa chachu ya maendeleo, kwa kuwa asilimia 34 ya uzalishaji wake wa umeme unatokana na gesi asilia.
“Tumejipanga kuhakikisha gesi inachochea ukuaji wa viwanda, upatikanaji wa nishati kwa wote, na maendeleo ya kiuchumi Afrika Mashariki,” amesema Mramba.
Kutokana na hilo, Mramba amesema maendeleo ya LNG, masoko ya gesi ya ndani, na ushirikiano wa kibiashara wa kikanda ni miongoni mwa mada kuu itakayojadiliwa katika EAPCE’25.
Naye mdau mmoja wa masuala ya gesi ambaye ameomba jina lihifadhiwe kwa kuwa si msemaji wa kampuni yake, amesema ili kufanikisha mipango ya kuongeza uwekezaji katika sekta ya mafuta na gesi, Afrika Mashariki inahitaji sera madhubuti na ushirikiano wa kikanda.
Amesema Tanzania na Msumbiji tayari zimeanzisha sheria maalum za kusimamia uchimbaji wa gesi, huku Kenya na Uganda zikiharakisha maboresho ya sera zao ili kuvutia wawekezaji zaidi.
Hata hivyo, Mramba amesema majadiliano kuhusu uratibu wa sera miongoni mwa nchi za EAC yatalenga kuunda mazingira thabiti ya uwekezaji na maendeleo endelevu ya sekta hiyo.
Amesema mbali na mafuta na gesi, mkutano huo pia utajadili mbinu za mpito wa nishati safi, nafasi ya gesi kama nishati mbadala, na jinsi Afrika Mashariki inavyoweza kushiriki kikamilifu katika soko la kimataifa la nishati.
“Pamoja na matarajio ya kusainiwa kwa mikataba muhimu na kutangazwa kwa miradi mipya ya uwekezaji, mkutano huu unatarajiwa kuwa na matokeo makubwa kwa mustakabali wa sekta ya nishati katika kanda,” amesema katibu mkuu huyo.