
Madaba. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema hakuna mwananchi atakayeguswa na mradi unaotekelezwa na Serikali asilipwe fidia.
Ingawa inaweza kuchelewa, amesema Serikali itahakikisha inampa kila mwananchi haki yake anayostahili.
Rais Samia ametoa hakikisho hilo la fidia kwa wananchi wakati akijibu ombi la Mbunge wa Madaba (CCM), Dk Joseph Mhagama aliyeomba wananchi watakaopitiwa na ujenzi wa Barabara ya Makambako walipwe fidia.
Rais Samia amesema hayo leo Jumanne, Septemba 24, 2024 alipozungumza na wananchi wa Madaba mkoani Ruvuma, ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya siku sita mkoani humo aliyoianza jana Jumatatu.
“Hakuna mradi utakaopita kwa wananchi, Serikali ichukue ardhi bila kulipa fidia za watu. Inaweza ikachelewa lakini sio kwamba Serikali itaacha kabisa kulipa fidia,” amesema Rais Samia.
Hata hivyo, amesisitiza uzalishaji zaidi kupitia shughuli mbalimbali kikiwamo kilimo ili kujijengea uwezo Serikali wa kutekeleza miradi mingi kwa fedha zake za ndani, hivyo kulipa fidia haraka.
“Lakini niwahakikishie hakuna mwananchi atakayedhulumiwa, kila mmoja atakayepitiwa na mradi atalipwa fidia yake,” amesema.
Sambamba na hilo, Rais Samia amemtaka Waziri wa Maji, Jumaa Aweso kuhakikisha Mradi wa Maji wa Mtyangimbole unakamilika baada ya miezi mitatu.
Amesema uwekaji wa jiwe la msingi katika mradi huo kunaibua matumaini ya wananchi, ni vema kuhakikisha maji yanapatikana haraka.
Amesema matarajio yake kufikia mwakani Serikali itahakikisha upatikanaji wa huduma ya maji unafika asilimia 85 kwa vijijini na zaidi ya 90 kwa mijini.
Utekelezaji wa hilo, amesema ni kuakisi maelekezo ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020/25.
Rais Samia amesema hayo baada ya kuweka jiwe la msingi katika Mradi wa Maji wa Mtyangimbole kwa niaba ya miradi mingine 30 inayotekelezwa Madaba.
Amewasihi wananchi kuhakikisha wanatunza vyanzo vya maji ili kulinda uhai wake.
Awali, akizungumza katika mradi huo, Waziri Aweso amesema hadi sasa upatikanaji wa maji vijijini ni asilimia 79, huku mijini ikiwa ni asilimia takriban 90.
Kwa kuwa kuna miradi inayoendelea kutekelezwa, amesema itakapokamilika, vijijini upatikanaji wa huduma hiyo utafikia asilimia 85 na mjini zaidi ya 90.
Endelea kufuatilia Mwananchi kujua kinachoendelea kwenye ziara hiyo