Angola. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema bara la Afrika linahitaji mshikamano wa pamoja ili liweze kuwa imara na kuheshimika.
Samia aliyasema hayo jana Jumanne, Aprili 9, 2025 wakati akilihutubia Bunge la Angola akiweka historia ya kuwa Rais wa kwanza mwanamke kulihutubia Bunge hilo.
“Giza linaloonekana katika bara letu ni kielelezo kuwa tunahitaji kuwa na mshikamano utakaozifanya nchi zetu kuwa imara,” amesema.

Amesema mshikamano utakaooneshwa na nchi za bara hilo, sio tu kupambana na umaskini, bali pia utalifanya kuheshimika.
Rais Samia alilihutubia bunge hilo akiwa katika siku ya pili ya ziara yake nchini humo, ambayo ataihitimisha leo Jumatano, baada ya kupewa heshima ya kulihutubia na Spika wa Bunge wa nchi hiyo ambaye pia ni mwanamke, Caroline Carqueira.
Aidha, Rais Samia amesema wamekubaliana na Rais mwenzake wa Angola, Joao Goncalves Lourenco kushirikiana na kuhakikisha changamoto zinazozikumba nchi hizo mbili zikiwamo za kuimarisha uchumi wanapambana nazo, ili kuleta maendeleo si ya nchi hizo tu bali kwa bara zima la Afrika.
Amempongeza Rais Lourenco kwa kuimarisha uchumi wa nchi yake na kupambana na rushwa na kuwataka wananchi wa nchi hiyo, kuendelea kumuunga mkono rais wao katika mapambano hayo.
Rais Lourenco amesema uchumi wa Angola hivi sasa unafikia Dola 100 bilioni za Marekani (Sh266.6 trilioni) na umelifanya taifa hilo kuwa na uchumi imara unaotokana na biashara ya mafuta na madini.
Ziara ya Rais Samia nchini Angola ni ya kuimarisha uhusiano wa nchi hizo mbili uliojengwa na waasisi hayati Baba wa Taifa, Julius Nyerere na hayati Agustino Neto wakati wa harakati za ukombozi wa nchi ya Angola.
Rais Samia ametembelea nchi hiyo baada ya kupita miaka 19 tangu Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete alipotembelea nchi hiyo mara ya mwisho mwaka 1996.
Rais Samia amesema Tanzania ina fursa nyingi za uwekezaji na amewakaribisha wananchi wa Angola kuitembelea na Watanzania kutafuta fursa nchini humo.

Amesema Tanzania ina hazina kubwa ya gesi na madini ambayo bado haijatumika vya kutosha.
“Nikupongeze Spika wa Bunge, Caroline kwa kuwa mfano mzuri wa kuliendesha Bunge hili kidemokrasia, huu ni mfano wa kuigwa,” amesema Rais Samis.
Ameahidi kuwa katika ziara yake ambayo ameambatana na baadhi ya wabunge, itaendeleza uhusiano wao wa kutembeleana na anawaruhusu kufanya hivyo.
Aidha, amesema Tanzania kihistoria ilisimama imara kuisaidia Angola kwa juhudi zake za kupambana na utawala wa kikoloni ndio maana kuna baadhi ya maeneo yamepewa majina ya wapigania uhuru wake.

Rais Samia amesema nchi za Afrika bado zina changamoto ya ulinzi na usalama ndiyo maana katika hati za makubaliano walizotiliana saini jana, suala la usalama limepewa kipaumbele.