Mwanga. Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amezindua mradi mkubwa wa maji wa wilaya tatu za Same- Mwanga- Korogwe ambao utanufaisha wananchi zaidi ya 456,931.
Mradi huo chanzo chake ni Bwawa la Nyumba ya Mungu, ulianza kutekelezwa mwaka 2014 na sasa awamu ya kwanza imekamilika ukiwa umegharimu zaidi ya Sh300 bilioni.
Hatua hii imefikiwa baada ya Machi 21, 2024 wakati Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango wananchi wa wilaya hizo baada ya kutembelea mradi huo, kwamba endapo maji hayangetoka hadi Juni 2024, angeachia ngazi.

“Amri ya Rais (Samia Suluhu Hassan) ni kwamba maji yatoke Mwanga na Same ifikapo Juni mwaka huu, nataka nirudie tena, mjipange vizuri, wasimamieni makandarasi na wataalamu, bahati nzuri wana uwezo, usiku na mchana maji yatoke. Mradi huu umekuwa kero kwa wananchi wa maeneo haya, ni takribani miaka 19 imepita tangu umeahidiwa na kuanza kutekelezwa 2014,” alisema Dk Mpango.
Hata hivyo, maji hayakutoka muda huo na zilikuwepo taarifa zilizobainishwa na Rais Samia kuwa Dk Mpango alishaandika barua akitaka kuachia ngazi, ingawa hakueleza kama sababu zinahusiana na mradi huo.
“(Mpango) ana sababu kadhaa lakini siyo za mahusiano ya kazi. Ana miaka 68 na angependa kuishi zaidi ikiwezekana agonge 90 huko. Aliniambia mama yake aliyemzaa alifika 88 na angependa ampite mama yake kidogo asogee mbele.
“Sasa (akaniambia) hizi pilika mnazoniingiza sitafika huko. Naomba nipumzisheni. Nikambishia-bishia, wiki iliyopita hapa akanikabidhi barua yangu hii. Kama hunijibu kwa mdomo barua yangu hii na barua pia sikumjibu…,”alieleza Rais Samia katika mkutano huo uliofanyika Januari 19, 2025 na ambao ulimchagua Rais Samia kuwa mgombea urais uchaguzi mkuu 2025 na Balozi Emmanuel Nchimbi kuwa mgombea mwenza.
Historia inaonyesha mradi huo wa maji ulitolewa ahadi na Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete Mei 29, 2005 wakati akiomba kura kuingia madarakani kwa kipindi cha kwanza.
Uzinduzi wa mradi huo umefanywa leo Jumapili, Machi 9, 2025 na Rais Samia na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Waziri wa Maji, Jumaa Aweso na Waziri Mkuu mstaafu, Cleopa Msuya.
Msuya ambaye ni mkazi wa Mwanga, alikuwa amekaa kwenye kiti mwendo na inaelezwa alikuwa miongoni mwa wana Mwanga na Kilimanjaro waliokuwa wakiupigania mradi huo ili ukamilike.
Akizungumza kabla ya Rais Samia kuuzindua, Waziri Aweso amesema chanzo hicho cha maji kina uwezo wa kuchukua lita milioni 103 za maji wakati mahitaji ya maji Same na Mwanga ni lita milioni sita.
“Leo tumekamilisha kazi kubwa na nzuri uliyoifanya Rais, eneo hili ni la chanzo na linaweza kuchukua maji lita milioni 103, mahitaji ya Mwanga na Same ni lita milioni 6, huu ni mradi mkubwa sana wa kumaliza tatizo la maji,” amesema Aweso.
Awali, akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu amesema mradi huo ni wa kitambo, jiwe la msingi la ujenzi wake liliwekwa na Rais Samia alipokuwa Makamu wa Rais.

Baada ya awamu ya kwanza kukamilika, amesema tayari wananchi wa Wilaya ya Mwanga wanapata maji kwa asilimia 89.
Sambamba na hilo, amesema katika mkoa huo kuna hali shwari ya kisiasa, huku akirejea matokeo ya uchaguzi wa serikali za mitaa, ambako CCM ilieshinda kwa asilimia 98.25.
Katika Wilaya za Same na Mwanga, amesema CCM ilishinda uchaguzi huo kwa asilimia 100 na kwamba wakuu wote wa wilaya hizo ni wanawake.
“Wamefanya hiyo kwa sababu ya mapenzi makubwa na wewe umetuletea fedha nyingi za maendeleo. Miradi 1,360 ya maendeleo imefanywa katika nyanja zote,” amesema.
Kati ya miradi hiyo, amesema huo wamaji wa Same-Mwanga-Korogwe ni mmoja wapo.
Amesema kama ilivyofanyika katika uchaguzi wa serikali za mitaa, hali itakuwa hivyo hata kwenye Uchaguzi Mkuu Oktoba 2025.
Walichokisema wananchi
Baadhi ya wananchi wa Mwanga wakizungumza na Mwananchi, wamesema kukamilika kwa mradi huo ni faraja kubwa kwao kwa kuwa wameondokana na adha ya kutembea umbali mrefu kusaka maji na kutumia maji yasiyo safi na salama.
Leonard Mapunde, amesema tangu mwaka 1976 alipohamia Mwanga, wamekuwa na changamoto kubwa ya maji safi na salama.

“Tangu mwaka 1976 hadi sasa ni zaidi ya miaka 40 upatikanaji wa maji ulikuwa ni mgumu sana, kipindi hicho haya maji unayoyaona hayakuwepo, watu wa kijiji hiki na vijiji jirani tunashukuru sana Serikali kwa mradi huu,” amesema Mapunde.
Monica Abdalla amesema walikuwa wakitembea umbali mrefu kutafuta maji ambayo pia hayakuwa salama, jambo ambalo lilisababisha washindwe kufanya shughuli nyingine za maendeleo.
“Ilikuwa ukiishiwa na maji kwenda kuyafuata ni ngumu kwani ni mpaka upande mlima ndio utayakuta maji nyuma ya mlima, na maji hayo kukiwa na upepo yanachafuka, lakini pia yalikuwa yanakuwa machafu kwa sababu watu wanajisaidia humo, kila kitu watu wanafanya humo kwa hiyo tukawa tunayatumia tu kwa kuwa hatuna jinsi,” amesema.
“Huu mradi unatusaidia sana, tunamshukuru mama kwa kutukumbuka, kwani unatusaidia, ukiwa na shida hata kama ni jioni unapata maji karibu na nyumbani na unaandaa chakula bila shida, tofauti na hapo nyuma ambapo hata kuoga ilikuwa ni shida, tulikaa hata siku mbili bila kuoga. Tunamshukuru sana mama kwa kutuondoa kwenye ugumu na changamoto ya maji tuliyokuwa nayo,” amesema Monica.
Naye Gifteli Ngowo amesema kwa sasa wanaishi maisha ya amani na furaha kwa kuwa maji yanapatikana bila shida na watahakikisha wanautunza mradi huo ili uweze kuwa endelevu.

Rais Samia Suluhu Hassan leo Jumapili, Machi 9, 2025 amezindua mradi wa maji wa Same -Mwanga – Korogwe katika mikoa ya Kilimanjaro na Tanga. Uzinduzi huo uliofanyika Mwanga mkoani Kilimanjaro, pia umeshuhudiwa na Waziri wa Maji, Jumaa Aweso na Waziri Mkuu mstaafu, Cleopa Msuya.
“Kwa sasa hivi huu mradi unatusaidia sana kwa sababu kwa umbali tuliokuwa tunatoka hapa kwenda kuchukua maji, ni umbali mrefu, kwa kweli namwambia mama asante sana, kwa hiki alichotutendea katika kijiji cha njiapanda Mwanga,” amesema Ngowo.
“Tutaendelea kuitunza hii miundombinu ya miradi ya maji ili iwe endelevu na iendelee kutusaidia tusiteseke tena kama kipindi cha nyuma. Hatutakubali kuona mtu akiharibu tukamuacha, yeyote atakayeharibu tutamripoti kwenye vyombo husika, tutahakikisha tunautunza kwa nguvu zote ili tusirudi tulikotoka,” amesema.
Endelea kufuatilia Mwananchi ambapo Rais Samia atahutubia mkutano wa hadhara Mwanga