Rais Samia awafunda wasanii ishu ya kugombana

Dar es Salaam. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amewataka wasanii kuacha tabia ya kugombana badala yake wakae chini kuzungumza na kusameheana.

Rais Samia ameyasema hayo Februari 22, 2025 katika hafla ya ugawaji tuzo za Tanzania Comedy Award, zilizotolewa katika ukumbi wa The Super Dome jijini Dar es Salaam ambako alihudhuria kama mgeni rasmi.

“Wakati naingia niliambiwa hawa watu wapo kama Simba na Yanga. Wanashindana wengine wana uhasama, lakini leo hapa wote wameacha tofauti zao na wamekuwa wamoja. Sehemu hii ni faida moja ya shughuli hii na amesema Leonardo hapa, kwamba kuwepo sote kwenye holi moja huu ni umoja wa Kitanzania.

“Nizungumze na wasanii haina maana kugombana. Kama wanadamu kutofautiana kupo hata mzaliwe tumbo moja, lakini tusitofautiane kama Watanzania, tutofautiane kama wasanii na tofauti inapokwisha turudi tuwe wamoja kama watanzania. Hivyo viugomvi ugomvi huko kwenye mitandao haviwapi tija, wanangu kaeni semeshaneni muendelee,” amesema Rais Samia.

Hata hivyo, Rais Samia ameahidi serikali kuendelea kuwashika mkono wachekeshaji nchini ili wafike Kimataifa.

“Tasnia hii ilitumika kufikisha jumbe mbalimbali muhimu kwa jamii. Baadhi yetu tunamkumbuka mzee Jangala alivyokuwa akitoa mafunzo kwa njia ya ucheshi. Ikiwemo kuhusu malezi ya watoto wetu.

Vilevile wengi tunakumbuka kundi la The Comedy walivyotumia ucheshi kutoa tahadhari kuhusu vishoka, na waliwaonesha vishoka wanapigwa shoti mara kwa mara,” amesema Rais Samia.

                     

Katika usiku wa tuzo hizo, wasanii kama Mama Mawigi, TX Dulla, Ndaro na Steve Mweusi  wamefanikiwa kuondoka na tuzo.