Rais Samia atoa neno ushirikishwaji sekta binafsi bandarini, mapato yakiongezeka

Unguja. Rais Samia Suluhu Hassan amesema ushirikishwaji wa sekta binafsi katika uendeshaji wa bandari na miundombinu mingine umechangia mafanikio makubwa nchini, ikiwemo ongezeko la mapato.

Amesema kati ya Julai hadi Februari mwaka 2024/25, mapato ya bandari na ushuru wa forodha yamefikia Sh8.26 trilioni, ikilinganishwa na Sh7.08 trilioni mwaka 2023/24.

Aidha, gharama za uendeshaji wa Bandari ya Dar es Salaam zimepungua kwa asilimia 30, kutoka Sh975 bilioni hadi Sh685.1 bilioni.

Hayo yamesemwa leo, Jumatano Aprili 30, 2025, na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla alipokuwa akisoma hotuba ya Rais Samia katika mkutano wa kimataifa wa Shirikisho la Vyama vya Mawakala na Forodha Afrika Mashariki na Kati (Fiata Rame).

Rais Samia amesema ushirikiano baina ya Serikali na sekta binafsi umeongeza ufanisi katika bandari.

“Muda wa kusubiri meli umepungua kutoka wastani wa siku 46 hadi saba kwa meli za mizigo mchanganyiko, huku muda wa kuhudumia meli za makasha ukishuka kutoka siku 10 hadi tatu,” amesema Rais.

Amesema wastani wa makasha yanayohudumiwa kwa mwezi umeongezeka kutoka 17,000 hadi 25,000, sawa na ongezeko la asilimia 47.

Rais Samia amesema Tanzania inanufaika na uhusiano mzuri na nchi wanachama wa Fiata, jambo linaloimarisha biashara na uwekezaji katika sekta ya uchukuzi.

Amesisitiza kuwa Tanzania ni lango kuu la mizigo kwa zaidi ya nchi nane za Afrika Mashariki na Kusini, na imeweza kuhudumia shehena kupitia bandari za Dar es Salaam, Tanga na Mtwara kwa kutumia barabara, reli na mifumo ya kisasa inayowaunganisha wadau wa usafirishaji.

“Miradi inayoendelea, Serikali inaboresha Gati namba 8 hadi 11 katika Bandari ya Dar ili kuhudumia meli kubwa, na inaendeleza ujenzi wa reli ya kisasa kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza na Kigoma,” amesema Rais.

Aidha, amesema miradi ya ukarabati wa viwanja vya ndege, barabara na vivuko inaendelea ili kuimarisha huduma za uchukuzi.

Kwa upande wa Zanzibar, Rais Samia amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imefanya maboresho katika sekta ya uchukuzi yaliyoleta matokeo chanya, ikiwemo ongezeko la meli za kigeni na uboreshaji wa huduma za mizigo.

“SMZ inaendelea kutekeleza miradi kama ujenzi wa miundombinu ya usafirishaji wa mafuta na gesi Mangapwani, bandari za Shumba Mjini, Kizimkazi, Wete na Mpigaduri, pamoja na ujenzi wa boti mbili za mwendokasi na vituo vya usafiri wa baharini,” amesema.

Akizungumzia ujenzi wa kiwanja kipya cha ndege Pemba, Samia amesema ujenzi unaendelea sambamba na marekebisho ya uwanja wa Abeid Amani Karume na barabara kuu za mjini na vijijini maeneo ya Unguja na Pemba.

Amesema mafanikio hayo yanaifanya Tanzania kuwa nchi bora ya biashara na ya kupitisha mizigo kimataifa.

Awali, akizungumza katika mkutano huo, Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa amesema mkutano huo unalenga kubadilishana maarifa, kuimarisha ushirikiano wa kisekta, kuchochea mageuzi ya kidijitali na kupunguza athari za kimazingira kupitia suluhisho bunifu.

Kwa upande wake, Rais wa Fiata, Turgut Erkeskin amesema hatua za Tanzania katika ujenzi wa reli na kuboresha bandari ni muhimu kwa maendeleo ya kikanda.

Amesisitiza kuwa mawakala wa forodha wana jukumu kubwa katika kuboresha mazingira ya biashara.

Naye, Rais wa Taffa, Edward Urio amesema Zanzibar sasa ni nembo ya biashara na ushirikiano wa sekta binafsi kama ule wa DP World, ambao umesaidia kuboresha bandari.

“Mafanikio zaidi yatawezekana kwa ubunifu na ushirikiano wa pamoja,” amesema Urio.

Rais wa ZFB amesema mkutano huo umeiweka Zanzibar katika nafasi ya kipekee kibiashara, kuelekea kuwa kitovu cha usafirishaji Afrika Mashariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *