Rais Samia atangaza kuongeza mishahara kwa wafanyakazi

Katika kuboresha hali na ustawi wa wafanyakazi nchini, Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ametangaza kuongeza kima cha chini cha mshahara kwa watumishi wa umma kwa asilimia 35.1.

Nyongeza hiyo itaanza kutumika Julai 2025 kwa kima cha chini kutoka Sh370,000 hadi Sh500,000 huku akitoa tumaini kwa ngazi nyingine pia zitapanda kwa kiwango kizuri kwa jinsi bajeti inavyoruhusu.

Ameyasema hayo leo Alhamisi Mei 1, 2025 wakati akihutubia maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani ‘Mei Mosi’ yanayofanyikia kitaifa mkoani Singida yenye kaulimbiu isemayo “Uchaguzi Mkuu 2025 utuletee viongozi wanaojali haki na masilahi ya wafanyakazi sote tushiriki’.

“Kwa watumishi wa sekta binafsi Bodi ya Kima cha Chini cha Mshahara inaendelea kufanya mapitio ili kuboresha kiwango cha chini cha mishahara,” amesema.

Rais Samia amesema hayo yote yametokana na kuangalia uchumi kupanda kutokana na nguvu za wafanyakazi ambapo umepanda kwa asilimia tano.

“Mwaka jana 2024, wakati tukiadhimisha siku hii Serikali ilisihi tuziongeze mishahara bali tukaendelea na kupandisha madaraja na masilahi mengine ya wafanyakazi, lakini mkakaza mkanda mkafanya kazi hadi uchumi ukakua.”

Kutokana na hilo Rais Samia amesema Serikali ikaangalia uchumi kupanda kutokana na wafanyakazi ndipo wametangaza kuongezeka kwa mishahara.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *