
Unguja. Rais Samia Suluhu Hassan ametoa wito kuwepo juhudi za pamoja katika kukabiliana na maradhi ya moyo.
Akizungumza kupitia hotuba yake iliyosomwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla katika mkutano wa pili wa kimataifa wa magonjwa ya moyo (Cardio Tan 2025), Rais Samia amesema takwimu zinaonesha ongezeko la maradhi hayo, hivyo hatua madhubuti zinahitajika.
Mkutano huo ulioandaliwa na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) umejumuisha wataalamu wa afya kutoka mataifa 52 ya Ulaya, Afrika na Amerika.
Rais Samia amesema kwa sasa duniani magonjwa ya moyo na shinikizo la damu yanaongoza kwa kusababisha vifo, yakichangia vifo vya watu milioni 20 kwa mwaka, sawa na wastani wa watu 50 kwa siku.
Amesema kwa Tanzania, inakadiriwa watu milioni 4.9 wanakabiliwa na magonjwa ya moyo, yanayochangia karibu asilimia 13 ya vifo vyote.
“Idadi hii ni kubwa na inatufanya tuimarishe mifumo yetu ya kuzuia na kutibu magonjwa haya,” amesema Rais Samia.
Hata hivyo, amesema Serikali za pande zote mbili za Muungano zitaendelea kutoa elimu juu ya madhara ya matumizi ya tumbaku, pombe na ulaji usiofaa, huku pia ikiimarisha diplomasia ya afya kwa kushirikiana katika utafiti na utoaji huduma za afya.
Amesema kauli mbiu ya mkutano huo ya “Kuimarisha huduma za moyo barani Afrika kupitia jitihada za pamoja,” inalenga kuhimiza ushirikiano wa kisekta na ubunifu ili kuboresha huduma na miundombinu ya afya.
Katika kuhakikisha huduma bora, Rais Samia ameahidi kuendeleza uwekezaji wa huduma za kibingwa, utafiti na ubunifu, sambamba na kutoa wito kwa wahudumu wa afya kuzingatia maadili ya taaluma yao.
Kwa upande wa lishe, Rais Samia ameitaka Maabara ya Taifa ya Utafiti wa Lishe kuendelea kutoa huduma bora ili kusaidia tafiti za lishe na kuchangia kupunguza magonjwa yasiyoambukiza.
Awali, akizungumza katika mkutano huo, Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dk Peter Kisenge amesema taasisi hiyo imeendelea kutoa huduma bora na sasa inafanya upasuaji wa moyo kwa wastani wa watu 3,000 kwa mwaka kwa kutumia teknolojia ya tundu dogo na zaidi ya watu 800 kwa upasuaji wa kifua wazi.
Amesema asilimia 52 ya watoto wanaofika katika taasisi hiyo hukutwa na matatizo ya moyo, wengi wakiwa nayo tangu kuzaliwa. Katika miaka minne iliyopita, watu 8,786 walipata matibabu ya moyo JKCI, wakiwamo watoto 365 waliopatiwa upasuaji mwaka 2023 pekee.
Kisenge amesema Serikali imewekeza zaidi ya Sh20 bilioni kwa vifaa na miundombinu ya taasisi hiyo, ikiwa ni pamoja na kuanzisha Chuma cha Uangalizi Maalumu (ICU) cha watoto chenye vitanda 16, kubwa zaidi Afrika.
Aidha, Dk Kisenge amesema zaidi ya watoto 500 kwa sasa wanahitaji upasuaji na wamepanga kuanzisha tawi la JKCI Zanzibar ili kupunguza usumbufu kwa wagonjwa kutoka visiwani.
Naye, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Zanzibar, Dk Mngereza Mzee Miraji amesema maradhi ya moyo na mishipa ya damu husababisha kati ya asilimia 13 hadi 18 ya vifo hospitalini.
“Hadi Machi 2025, Zanzibar ilikuwa na madaktari bingwa wa moyo watatu pekee na daktari bingwa mmoja wa upasuaji wa moyo,” amesema.
Katika mwaka wa fedha 2023/24, wagonjwa 571 walilazimika kusafirishwa nje ya Zanzibar kwa huduma maalumu, asilimia 20 kati yao walikuwa na matatizo ya moyo.
Kwa kipindi cha miaka 25 (1999–2023), wagonjwa 1,125 walifanyiwa upasuaji wa moyo, wengi wao wakiwa watoto waliotibiwa nje ya nchi.
Serikali ya Zanzibar inatumia takribani Sh1.5 bilioni kila mwaka kwa matibabu ya watoto wenye matatizo ya moyo kupitia JKCI.
Mkutano huo wa siku tatu unafanyika Zanzibar kuanzia Aprili 10 hadi 12, 2025, ukiwa ni wa pili kufanyika nchini na umejumuisha wataalamu kutoka mataifa 52 duniani.