Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amesema toleo jipya la Sera ya Mambo ya Nje ya Mwaka 2001 (Toleo la 2024), limekuja na maeneo tisa muhimu ambayo ni pamoja na kujielekeza kuimarisha diplomasia ya kiuchumi, kuvutia uwekezaji wa mitaji mikubwa na kutumia fursa ya kijiografia kunufaika na soko huru la biashara la Afrika.
Akizungumza leo Jumatatu, Mei 19, 2025, wakati wa uzinduzi wa Sera mpya ya Mambo ya Nje (Toleo la 2024) uliofanyika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam, Rais Samia sera hiyo pia inalenga kuleta uhimilivu wa uchumi wa nchi kwa kuongeza kasi na uwekezaji katika sekta binafsi, hususan kujizatiti na uwekezaji wa ubia ambao amesema bado Tanzania haifanyi vizuri.
“Hili linakwenda sambamba na kuongeza uwezo wa sekta binafsi ya ndani iweze kushiriki katika uwekezaji nje ya mipaka yetu,” amesema Rais Samia.

Rais Samia ametaja kuendelea kukuza hadhi ya nchi kwa kueneza mazuri yaliyopo kiuchumi, kisiasa, kijamii, utajiri wa utamaduni, mila na ustaarabu.
“Pia lugha ya Kiswahili itumike katika kupanua soko la ndani na nje ya Afrika sambamba na kukuza ushiriki waishio nje katika kuchagia maendeleo binafsi na nchi.”
Mabadiliko mengine ni kuangazia maeneo ya fursa mpya za ushirikiano na maendeleo ikiwemo sekta ya buluu, kijani na kidijiti na maeneo mengine ikiwemo sekta ya madini ya kimkakati ili kupanua mawanda ya uchumi wa Tanzania.
Rais Samia ametaja ushirikiano na nchi na mashirika ya mataifa mengine katika kupambana na changamoto za dunia ikiwemo majanga ya afya, matumizi mabaya ya teknolojia mpya, mabadiliko ya tabianchi, uhalifu unaovuka mipaka na ugaidi.

“Jambo lingine tutaongeza uwazi na uwajibikaji katika shughuli za kidiplomasia kwa kutumia diplomasia ya umma (Public Diplomacy) kwa kutumia mifumo ya kidijitali lengo ni kuifanya nchi itambue kazi zinazofanywa na mabalozi wetu wanaoiwakilisha nchi katika maeneo mbalimbali duniani,” amesema Rais Samia.
Huku akitaja kuwa Wizara ya Mambo ya Nje ndiyo mtekelezaji mkuu wa sera hiyo, Rais Samia amesema sera hiyo imezingatia ushirikiano wa kimataifa kwa upande wa Zanzibar huku akisema ni rasmi nchi inaenda kuangazia fursa za vijana ndani na nje ya nchi.
Rais huyo ameitaka wizara hiyo kutoa elimu ya sera hiyo kwa taasisi za umma kuhusu maudhui yake na namna yanavyogusa majukumu yao ya kila siku, huku akiagiza mabalozi wastaafu watumike kujenga uwezo na uelewa wa sera hiyo kwa umma.
“Hapa nimeona timu kubwa tu ya mabalozi wastaafu, lakini wamestaafu wakiwa bado wana nguvu wanaweza wakatumika kwenye kazi hii, mkawapangia kazi maalumu ya kukaa na sekta mbalimbali kwa sababu wizara mko ‘bize’ sana wao wakafanya kazi ya kutafsiri ile sera,” amesema.
Pia amewaagiza mabalozi wa Tanzania nje ya nchi kuisoma sera hiyo na kuielewa kisha kuanza kutangaza mabadiliko chanya ya sera hiyo, huku akidokeza kuwa inataka kuwepo diplomasia shirikishi kwa wananchi.

“Naziagiza wizara, idara zinazojitegemea, wakala za Serikali na tawala za mikoa na serikali za mitaa kuhakikisha mnajumuisha malengo na mikakati ya sera hii katika mipango mikakati yenu, na kuanza utekelezaji wake mara mwongozo utakapotolewa,” amesema.