
Peramiho. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amemtaka Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe kuchunguza madai ya wakulima wa kahawa kukatwa fedha kinyemela na vyama vikuu vya ushirika.
Amesema anatambua kuwepo kwa malalamiko hayo yaliyosababishwa na ongezeko la bei ya kahawa mwaka huu.
Rais Samia amesema hayo leo Jumanne, Septemba 24, 2024 alipozungumza na wafanyakazi na viongozi wa shamba la kahawa la Aviv Tanzania Limited, ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya siku sita mkoani Ruvuma.
“Ninatambua uwepo wa malalamiko ya wananchi kwamba, kwa sababu kahawa imepanda bei baadhi ya vyama vikuu vya ushirika (hakuvitaja) vinawakata wakulima kinyemela,” amesema.
Amemtaka Waziri Bashe afuatilie ili kuwa na mfumo wa wazi utakaowafanya wakulima kuona wanachouza na uhalisia wa makato yao.
“Huu ujanja ujanja unaoendelea unapaswa kukomeshwa,” amesema mkuu huyo wa nchi alipotembelea shamba hilo lenye ukubwa wa hekta 200.
Hata hivyo, amesema ongezeko la bei hiyo na malipo ya haraka kwa wakulima wa kahawa ni matokeo ya juhudi za Serikali za kuongeza ufanisi katika mauzo ya zao hilo.
Kadhalika, Rais Samia ameitaka wizara ya kilimo kujipanga vema na masharti yanayotolewa na masoko ya kimataifa ya kahawa hasa like la uzalishaji bila kukata misitu.
Pamoja na kutokata misitu, amesema masharti mengine ni kukagua, kuyasajili na kupeleka taarifa za mashamba kwenye masoko hayo ili ijulikane linakotoka zao husika.
“Wanatambua tusikate misitu, kweli kwao wameshakata lakini sisi tunataka soko, tunapaswa kuhakikisha tunayatimiza masharti ili kupata soko,” amesema.
Amewataka wakulima watumie fursa ya uwepo wa bei kubwa ya kahawa mwaka huu kuhifadhi fedha, ili wasitaabike katika nyakati ambazo bei ya zao hilo itashuka.
“Misimu ikiwa mizuri na bei ikiwa nzuri tuwe na mifumo ya kujiwekea akiba ili mabadiliko ya tabianchi yanapotokea tuwe na akiba,” amesema.
Katika hatua nyingine, Rais Samia ameutaka uongozi wa shamba hilo, unaofanya shughuli za kijamii ujikite katika uchimbaji wa visima vya umwagiliaji kwenye mashamba ya wakulima.
Amesema kufanya hivyo, kutawawezesha wakulima kuzalisha kahawa kwa umwagiliaji na kuuza kwa Aviv.
Awali, akizungumza katika ziara hiyo, Waziri Bashe amesema shamba hilo ni moja kati ya 50 yanayozalisha kahawa na kwamba hilo ni kubwa zaidi ya mengine yote.
Amesema asilimia 60 ya kahawa inayozalishwa na shamba hilo inauzwa nje ya nchi kwa Kampuni ya Strabag.
Hata hivyo, amesema wastani wa bei ya kahawa mwaka huu ni Dola 4.3 za Marekani, kiwango ambacho ni tofauti na nyakati zilizopita.