
Dodoma. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ametia saini marekebisho ya sheria saba, ikiwemo Sheria ya Uwekezaji wa Maeneo Maalumu ya Kiuchumi namba 6, 2025, ambayo pamoja na mambo mengine, inafuta rasmi Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na Mamlaka ya Kukuza Mauzo ya Bidhaa Nje ya Nchi (EPZA).
Sheria hiyo inafuta mamlaka hizo na kuanzisha Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalumu ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA), ambazo zilibainika kuwa majukumu yake kuingiliana na kushabiana.
Aidha, hatua ya kusainiwa kwa Sheria ya Marekebisho ya Sheria za Kazi namba 4 ya mwaka 2025 kunamaanisha sasa likizo ya uzazi kwa mwajiriwa atakayejifungua mtoto njiti imejumuisha muda uliobaki kufikia wiki za ujauzito, huku baba akipewa siku saba za kupumzika.
Kutiwa saini kwa sheria hizo kumetangazwa bungeni leo Jumanne Aprili 8, 2025 na Naibu Spika wa Bunge, Mussa Zungu, alipokuwa akisoma taarifa ya Spika wa Bunge.
Zungu amesema miswada hiyo saba ilipitishwa na Bunge katika Mkutano wa 18 wa Bunge na kuwataarifu wabunge kwamba miswada hiyo imepata kibali cha Rais Samia na sasa inajulikana kama sheria.
Ametaja sheria zilizopata kibali cha Rais Samia ni Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali namba 1 wa Mwaka 2025, Sheria ya Marekebisho namba 2 ya mwaka 2025 na Sheria ya Utangazaji Tanzania wa mwaka namba 3 mwaka 2025.
Nyingine ni Sheria ya Marekebisho ya Sheria za Kazi namba 4 ya mwaka 2025, Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Usimamizi wa Mazingira namba 5 ya mwaka 2025, Sheria ya Uwekezaji wa Maeneo Maalumu ya Kiuchumi namba 6 ya mwaka 2025.
Nyingine ni Sheria ya Kuidhinisha Matumizi ya Nyongeza ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2024/2025 namba 7 ya mwaka 2025.