Dar es Salaam. “Kahawa ni kinywaji kinachotuliza akili”, hii ni ya matamshi ya kwanza aliyoyatoa Rais Samia Suluhu Hassana leo Februari 22, 2025 wakati akifungua mkutano wa tatu wa nchi zinazozalisha kahawa barani Afrika uliofanyika kwa siku mbili jijini Dar es Salaam.
Akiwa mwenye bashasha baada ya kunywa kikombe cha kahawa alicholetewa muda mfupi baada ya kuanza hotuba yake Rais Samia alishindwa kuficha mapenzi yake dhidi ya kinywaji hicho na kueleza anavyokipenda
“Kahawa ni tamu sana, ni kinywaji ambacho kinatuliza akili kwa wale wanywaji wa kahawa kama mimi ikitokea asubuhi hujapata kikombe unakuwa hujajisikia kama umeamka. Kama hapa nilivyokunywa ndiyo nasikia akili imekaa sawa.
“Takwimu zote zinaonesha kwamba watu wanakunywa vikombe bilioni 3 vya kahawa kwa siku. Kati ya vikombe hivyo vipo vikombe vyenye kahawa nzuri inayozalishwa na wakulima wa kahawa barani Afrika ambao wengi wao ni wakulima wadogo,” amesema Rais Samia.

Hata hivyo kiongozi huyo Mkuu wa Tanzania amesema licha ya uhitaji wa zao hilo kuendelea kuwa mkubwa duniani bado bara la Afrika halijaitumia vyema fursa ya kuwa mzalishaji.
Amesema Afrika imepoteza hadhi yake kwenye sekta ya kahawa duniani ikilinganishwa na ilivyokuwa miaka ya 1960 ambapo uzalishaji wa zao hilo ulifikia asilimia 25 ya kahawa yote inayozalishwa duniani.
“Sasa hivi uzalishaji wetu umeshuka hadi kufikia asilimia 11. Tumeshuka licha ya soko la kahawa duniani kuendelea kukua na nchi mbalimbali kuongeza uzalishaji. Tunahitaji kuongeza uzalishaji na kurejesha nafasi tuliyokuwa nayo katika biashara ya kahawa duniani.
Amezitaja miongoni mwa changamoto zinazosababisha kushuka uzalishaji wa zao hilo ni kutotabirika kwa bei hali inayosababisha wakulima wa kahawa kukata tamaa na kugeukia kwenye mazao mengine.
Changamoto ya pili aliyoitaja ni kahawa kutoongezwa thamani barani Afrika akieleza kuwa nchi nyingi zinaishia kuzalisha kahawa ghafi.
“Huwa tunalima na kuishia kusafirisha kahawa ghafi ikienda huko inaongezwa thamani na kufungashwa na vizuri kisha inarudishwa kuuzwa kwetu kwa gharama kubwa. Hili linapaswa kufanyiwa kazi, Serikali zetu zinapaswa kufanya jitihada kubwa kuwapa nguvu wazalishaji na wanaoongeza thamani”.
“Zaidi ya asilimia 90 ya mapato ya zao la kahawa inayozalishwa Afrika inakwenda nje ya bara hili, wazalishaji ni sisi lakini faida inakwenda kwingine. Kuuza malighafi nje kunaondoa kazi kwa vijana wetu, hivyo hatuna budi kuweka nguvu na kufanya sekta ya kahawa ikue na sisi kuwa sehemu ya kuleta ushindani kwenye soko la kahawa duniani”.

Changamoto nyingine aliyotaja ni kiwango kidogo cha biashara baina ya nchi za Afrika zenyewe akieleza kuwa licha ya nchi hizo kuwa wazalishaji wakubwa wa kahawa na zaidi ya asilimia 90 ya kahawa kuzalishwa Afrika, nchi nyingi za bara hilo zinaagiza kahawa kutoka mabara mengine.
“Ni vyema tukafikiria jinsi ya kuzalisha kahawa, kuiongezea thamani na tukauziana wenyewe ndani ya bara la Afrika. Takribani magunia 12.3 milioni ya kahawa iliyosindikwa huingizwa barani Afrika hii ni sawa na asilimia 12 ya kahawa yote iliyoongezewa thamani duniani, hii ina maana kuwa Afrika kuna soko zuri la kahawa,” amesema.