
Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amefanya uteuzi wa nafasi mbalimbali pamoja na kupangia vituo vya kazi mabalozi ambapo Balozi Mobhare Matinyi amepangiwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Sweden.
Kabla ya uteuzi huo, Balozi Mobhare aliwahi kuwa Msemaji Mkuu wa Serikali ambapo Desemba 8, 2024 aliteuliwa kuwa balozi lakini hakupangiwa kituo cha kazi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Sharifa Nyanga leo Jumanne, Machi 25, 2025, Rais amefanya uteuzi wa viongozi mbalimbali na kuwapangia vituo mabalozi.
Taarifa hiyo inayomnukuu Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Moses Kusiluka, pia imeonyesha Balozi Hamad Khamis Hamad amepangiwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Msumbuji.
Rais amemteua Rachel Stephen Kasanda kuwa Mkuu wa Wilaya ya Masasi. Kasanda anachukua nafasi ya Lauteri John Kanoni ambaye uteuzi wake umetenguliwa.
“Profesa Jafari Ramadhani Kideghesho ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Mfuko wa Uhifadhi na Wanyamapori Tanzania. CPA Ashraph Yusuph Abdulkarim ameteuliwa kuwa Meneja Mkuu wa Shirika la Masoko Kariakoo,” imeeleza taarifa hiyo.