Rais Samia afanya uteuzi, amgusa Profesa Nagu, Mbungo

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amefanya uteuzi wa viongozi mbalimbali akimteua Profesa Tumaini Nagu kuwa Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), anayeshughulikia masuala ya afya.

Katika taarifa iliyotolewa leo Jumatatu Mei 19, 2025, na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Moses Kusiluka na kusainiwa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Sharifa Nyanga, mbali na Profesa Nagu, Rais Samia amemteua Dk Blandina Kilama kuwa Naibu Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, anayeshughulikia biashara na ubunifu.

“Dk Kilama anachukua nafasi ya Dk Lorah Madete ambaye uteuzi wake umetenguliwa na atapangiwa majukumu mengine,” imesema taarifa hiyo.

Wakati huohuo Balozi, George Madafa ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya Puma Energy Tanzania. Balozi Madafa anachukua nafasi ya Dk Majige Budeba ambaye amemaliza muda wake.

Pia, Jacob Kibona ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Bodi ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB) kwa kipindi cha pili, huku Meja Jenerali Mstaafu, John Mbungo ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Kampuni ya Meli Tanzania (Tashico), kwa kipindi cha pili.

Katika hatua nyingine, Rais Samia amemteua Mussa Hamza Mandia kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) kwa kipindi cha pili.

“Uapisho wa Naibu Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mtendaji utafanyika kwa tarehe itakayopangwa baadaye,” imesema taarifa hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *