Rais Pezeshkian: Iran itatoa jibu linalostahiki kwa uchokozi wa Israel dhidi yake

Rais Masoud Pezeshkian amesema kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haipendi vita lakini iko imara katika kujihami na kulinda usalama wa wananchi wake na itatoa jibu linalostahiki kwa uchokozi wa utawala wa Kizayuni dhidi yake.

Alfajiri wa Jumamosi ya tarehe 26 Oktoba 2024, utawala wa Kizayuni ulifanya uchokozi mpya kwa kujaribu kushambulia baadhi ya maeneo ya kijeshi ya mikoa ya Tehran, Khozestan na Ilam hapa Iran lakini shambulio hilo lilizimwa na mfumo imara wa ulinzi wa anga wa Jamhuri ya Kiislamu.

Taarifa ya Kituo cha Ulinzi wa Anga cha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kilisema kwenye taarifa yake kwamba shambulio hilo la Israel limezimwa na limesababisha madhara kiduchu tu.

Shirika la habari la IRIB limemnukuu Rais Masoud Pezeshkian wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran akisema katika kikao cha Baraza la Mwaziri kwamba kamwe Iran haitonyamaza kimya mbele ya uchokozi huo wa utawala wa Kizayuni dhidi yake.

Ameongeza kuwa, walimwengu wote wanashuhudia jinai za utawala wa Kizayuni kwenye Ukanda wa Ghaza na kusini mwa Lebanon na kwamba waungaji mkono wa jinai hizo wakiongozwa na Marekani wanapayuka kuwa wanalinda haki za binadamu lakini kila mmoja anaona jinsi wanavyoshiriki kikamilifu katika mauaji ya kutisha ya halaiki dhidi ya wanawake na watoto wadogo huko Palestina na Lebanon.