Rais Masoud Pezeshkian wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, jumuiya ya BRICS ikiwa na malengo yake makubwa imeweza kuwa kielelezo cha mafanikio cha ushirikiano kati ya nchi katika uga wa kimataifa.
Rais Pezeshkian amesema hayo katika hotuba yake kwenye Mkutano wa BRICS PLUS na kuongeza kuwa, ana matumai mazingira haya ya fikra za pamoja na kubadilishana mawazo yataandaa uwanja wa kuelekea kuanzishwa mfumo wenye uadilifu zaidi kwa msingi wa kuridhika pande zote.
Aidha amesemma kuwa, muuungano na uanzishaji wa mahusiano ya kirafiki ni matakwa ya nchi nyingi kwa minajili ya kujikwamua kutoka katika satuwa na udhibiti wa uchukuaji hatua kwa upande mmoja.
Rais wa Iran ameongeza kuwa: Misingi ya mfumo wa kambii moja imedhoofika sana na miundo mingi ya kimataifa kama vile Baraza la Usalama na Mfuko wa Fedha wa Kimataifa imepoteza ufanisi wake kutokana na ushawishi wa serikali za Magharibi.

Kadhalika amesema, ulimwengu bora ni mahali ambapo hakuna habari za vikwazo, vita, uchokozi, utaifishaji, na mauaji ya halaiki, na muelekeo wa pande kadhaa unachukua nafasi ya kuegemea upande mmoja, na akasema: Katika ulimwengu kama huo, kuna usawa badala ya ubaguzi, uwazi badala ya udanganyifu, na. mazungumzo badala ya vita.