
Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, ametoa salamu za rambirambi kufuatia shambulizi la kigaidi lililotokea kaskazini magharibi mwa Pakistan.
Katika barua yake ya rambirambi, Pezeshkian ameeleza masikitiko yake kwa serikali na taifa la Pakistan, pamoja na familia zilizopoteza wapendwa wao katika shambulio hilo.
Takriban watu 42 waliuawa na makumi ya wengine kujeruhiwa wakati kundi la magaidi wa kitakfiri lilipofyatulia risasi magari ya abiria yaliyokuwa yamewabeba Waislamu wa madhehebu ya Shia katika eneo la kaskazini magharibi mwa Pakistan.
Maafisa wa eneo hilo wa Pakistan walisema shambulio hilo lilitokea siku ya Alhamisi huko Kurram, wilaya yenye mandhari nzuri ya milimani katika mkoa wa Khyber Pakhtunkhwa, unaopakana na nchi jirani ya Afghanistan.
Hilo linahesabiwa kuwa moja ya mashambulizi mabaya zaidi katika eneo hilo katika miaka ya hivi karibuni dhidi ya jamii ya Waislamu wa madhehebu ya Shia nchini Pakistan.
Vikosi vya usalama vya Pakistan kwa sasa vinafanya oparesheni za kijasusi katika maeneo mbalimbali yasiyo na usalama nchini humo kuwasaka magaidi hao.