Rais wa Jamhuri ya Namibia, Mhe. Dkt. Netumbo Nandi-Ndaitwah amewasili nchini Mei 20, 2025 kwa ajili ya kuanza ziara rasmi ya siku mbili kuanzia tarehe 20 hadi 21 Mei, 2025.
Ziara hiyo ya kwanza kwa Mhe. Nandi-Ndaitwah kufanyika hapa nchini tangu kuingia kwake madarakani mwezi Machi 2025, inafuatia mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, Mhe. Dkt. Nandi-Ndaitwah amepokelewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo.
Akiwa nchini pamoja na mambo mengine, Mhe. Dkt. Nandi-Ndaitwah atafanya mazungumzo ya faragha na mwenyeji wake, Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan yatakayofuatiwa na mazungumzo rasmi ya kujadili namna ya kukuza ushirikiano baina ya nchi hizi mbili.
Kadhalika Viongozi hao kwa pamoja watazungumza na Waandishi wa Habari kuelezea makubaliano waliyofikia katika mazungumzo yao kabla ya kushiriki dhifa ya chakula cha jioni iliyoandaliwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa heshima ya Mhe. Dkt. Nandi-Ndaitwah.
Akiendelea na ziara yake nchini, Mhe. Rais Dkt. Nandi-Ndaitwah, Mei 21, 2025 anatarajiwa kutoa Mhadhara katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam pamoja na kutembelea Kituo cha Urithi wa Ukombozi wa Afrika kilichopo Dar es Salaam.
Tanzania na Namibia zimeendelea kuimarisha ushirikiano wa kihistoria ulioasisiwa na Waasisi wa mataifa haya mawili Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Hayati Sam Nujoma kupitia mikataba mbalimbali ya uwili na masuala yote yanayohusu Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
The post RAIS NETUMBO NANDI-DAITWAH AWASILI NCHINI TANZANIA appeared first on Mzalendo.