Rais Mwinyi kushiriki mkutano wa CTIS Uingereza

Unguja. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi, ameondoka nchini usiku wa kuamkia leo, Aprili 6, 2025, kuelekea jijini London, Uingereza, kwa ajili ya kushiriki Mkutano wa Biashara na Uwekezaji wa Jumuiya ya Madola (CTIS).

Mkutano huo wa kila mwaka, utakaofanyika katika Jumba la kihistoria la Jiji la London, unatarajiwa kuanza Aprili 7 na kumalizika Aprili 8.

Mkutano huu utawakusanya wafanyabiashara wa Jumuiya ya Madola, wakuu wa Serikali, mawaziri wakuu, na wawakilishi kutoka serikali mbalimbali za Jumuiya hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na CTIS, mkutano huu utakuwa jukwaa muhimu la kujadili vipaumbele vya biashara katika Jumuiya ya Madola.

“Tumelenga kufanya vikao vya jumla na majadiliano ya kiwango cha juu, pamoja na fursa za mitandao isiyo rasmi na mikutano ya moja kwa moja,” ilisema taarifa hiyo.

Mkutano huu utaweka msisitizo kwenye masuala ya kupunguza vizuizi vya biashara, kuvutia uwekezaji, kukuza masoko, pamoja na mabadiliko ya nishati duniani.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, zaidi ya wajumbe 400 kutoka nchi mbalimbali za Jumuiya ya Madola, wakiwemo wawekezaji, wafanyabiashara na watunga sera, watashiriki katika mijadala hiyo.

Mbali na kushiriki mkutano huo, Rais Mwinyi (ambaye amekwishafika nchini humo) atakuwa na mikutano na viongozi waandamizi wa Serikali ya Uingereza na taasisi zake.

“Atakutana na Watanzania wanaoishi Uingereza, na pia atakutana na Waziri Mkuu mstaafu wa Uingereza, Tony Blair, ambaye kwa sasa ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Tony Blair (TBI),” ilieleza taarifa hiyo.

Taasisi ya Tony Blair inashirikiana na viongozi wa kisiasa duniani kote ili kuwasaidia kuboresha maisha ya wananchi wao kwa kushauri kuhusu mikakati, sera na teknolojia.

Aidha, Rais Mwinyi atakutana na wadau wa uwekezaji katika sekta ya uchumi wa buluu, pamoja na sekta nyingine muhimu kama vile utalii, filamu, viwanda, nishati, na mafuta na gesi.

Kama sehemu ya ziara hiyo, Rais Mwinyi atashuhudia kusainiwa kwa makubaliano ya ushirikiano kati ya Wizara ya Uchumi wa Buluu na Chuo Kikuu cha Kent kwa ajili ya utafiti wa kilimo cha mwani.

Vilevile, atashuhudia kusainiwa kwa Mkataba wa Memorandamu (MoU) kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Kampuni ya Perry Engineering ya Uingereza kuhusu usambazaji wa mbegu za mwani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *