Unguja. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amesema ziara yake nchini Uingereza imekuwa ya mafanikio, hivyo baada ya muda mfupi Zanzibar itarajie kupokea wawekezaji katika sekta zinazoendana na sera ya uchumi wa buluu.
Amesema maeneo makuu matatu ambayo yanatarajiwa kupata uwekezaji ni utalii kwa upana wake, uvuvi na ukulima wa mwani na mafuta na gesi.
Dk Mwinyi aliondoka nchini Aprili 6, 2025 kuelekea Uingereza alikoshiriki mkutano wa Jumuiya ya Madola uliofanyika Aprili 7 na 8, ukijumuisha watunga sera, wakuu wa nchi na wafanyabiashara kutoka mataifa mbalimbali ukiwa na ajenda kuu ya uchumi wa buluu.
Aikiwa nchini humo alikutana na wafanyabiashara katika sekta za uchumi wa buluu, diaspora na Waziri mstaafu wa nchi hiyo, Tony Blair ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Tony Blair (TBI).
Akizungumza na waandishi wa habari leo Aprili 11, 2025 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Aman Karume, Rais Mwinyi amesema matarajio ya nchi baada ya muda mfupi ni kuanza kupokea wawekezaji katika sekta hizo.
Amesema kuna kampuni kubwa zimeonyesha na zina nia ya kutaka kuwekeza Zanzibar.
“Kwa hiyo, ziara yangu imepata kampuni nyingi ambazo zilikuwa tayari kuja Zanzibar. Kwa kukutana na hao wote matarajio yetu ni kwamba, baada ya muda mfupi wataanza kuja Zanzibar kama tulivyowaalika na wao kuwa tayari kuwekeza katika sekta hizo kuu za uchumi ambazo zinaenda sambamba na sera yetu ya uchumi wa buluu,” amesema.

Katika eneo la utalii, Dk Mwinyi amesema wamejitokeza wawekezaji wengi wenye nia ya kuwekeza Zanzibar.
Akizungumzia uvuvi na usafirishaji wa mwani, amesema wapo wenye hamu ya kwenda Zanzibar kuwekeza katika masuala ya uvuvi, lakini zaidi kuongeza thamani ya mwani.
Dk Mwinyi amesema wamekutana na kampuni za kutafuta data za mafuta na gesi na kuzitangaza duniani ili kampuni kubwa zifike kufanya tafiti kwenye maeneo ya mafuta na gesi.
Katika ziara ya siku nne, Dk Mwinyi amesema wamesaini mikataba ya ushirikiano.
Kati ya hiyo, amesema kuna kampuni inayolenga kuwekeza katika mnyororo wa thamani wa mwani ili kupata mbegu bora, kupambana na magonjwa na kusaidia utafiti kuhusu zao hilo.
“Pamoja na uwekezaji tumezungumza kujenga uwezo wa watu wetu, bila shaka vijana ndio walengwa wakuu na watapata fursa hizo,” amesema.
Kuhusu diaspora, amesema wapo tayari kuchangia uchumi wa nchi kwa namna mbalimbali kupitia uwekezaji.
“Wapo ambao wapo tayari kuchangia uchumi kwa fedha zao lakini wengine kuchangia kwa kushawishi na kuwa mabalozi wa kushawishi kampuni zije kuwekeza Zanzibar,” amesema.
Hata hivyo, amesema wametaja changamoto zinazowakabili ni pamoja na vitambulisho wakieleza kwa Zanzibar wanapata vitambulisho maalumu lakini pia wamekuwa wakipata Vitambulisho vya Taifa (Nida).
“Changamoto iliyopo Nida wanaweza kuwa wanaenda kule wanawapatia vitambulisho lakini wakataka kadi za diaspora nazo wazipate kulekule jambo ambalo tumelipokea,” amesema.
Akizungumzia hoja ya uraia pacha, amesema kama walivyokubaliana katika Serikali, wanapaswa kupewa hadhi maalumu kwa hiyo amewaeleza wizara husika ya Mambo ya Nje na Ushirkiano wa Afrika Mashariki imeshaanza mchakato wa kuwapa hadhi maalumu.
Amesema taarifa ni kwamba, mchakato umemalizika ndani ya Serikali na tayari umeshapelekwa bungeni.
Dk Mwinyi amesema hadhi maalumu itawapa fursa mbalimbali, zikiwamo bima ya usafiri na changamoto za familia zao ambazo wengine wameoa nje kwa hiyo zitatambulika.
“Hivyo, kwa ufupi nimewaeleza mchakato wa kuwapatia hadhi maalumu umeshafika pazuri na upo bungeni kwa hiyo changamoto zao zitaondoka,” amesema.