Unguja. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, amesisitiza umuhimu wa kudumisha amani, hasa katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu Oktoba mwaka huu.
Amesema kila mmoja anapaswa kuiombea dua nchi ili mchakato wa uchaguzi mkuu upite kwa amani na mshikamano.
Akizungumza leo Jumatatu, Machi 31, 2025, katika Baraza la Idd lililofanyika Polisi Ziwani, Unguja, baada ya Sala ya Idd el-Fitr, Dk Mwinyi amewahimiza wananchi kuendelea kudumisha umoja kwa ajili ya maendeleo ya Taifa.
“Tunamuomba Mwenyezi Mungu atujaalie kuendelea kuwa wamoja na kushirikiana kwa manufaa ya nchi yetu. Tuvuke kipindi hiki kwa salama ili kizazi cha sasa na kijacho kifurahie ustawi wa Taifa letu,” amesema Dk Mwinyi.

Viongozi wakuu wa kitaifa wakiwa katika swala ya Eid kitaifa iliyofanyika katika msikiti wa Zinzibar Mazizini Unguja.
Akiwahutubia waumini wa Kiislamu pamoja na viongozi wa kitaifa waliopo madarakani na wastaafu, Rais Mwinyi ameendelea kusisitizia umuhimu wa kuendeleza matendo mema yaliyotekelezwa katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, ikiwa ni pamoja na kusaidia wenye uhitaji.
“Yote tuliyotekeleza katika mwezi mtukufu, tuyaendeleze, hatupaswi kuyaacha kwa sababu tu mwezi mtukufu umeisha,” amesema Rais Mwinyi.
Amesema utoaji wa zaka na sadaka ni miongoni mwa mafundisho ya Kiislamu yenye faida kubwa kwa jamii, kwa kuwa huchochea upendo, mshikamano na huondoa chuki na husuda miongoni mwa watu.
“Haya ni mambo muhimu yanayojenga jamii imara na kuleta maendeleo. Ukarimu na huruma ni misingi ya uhai wa jamii yenye mshikamano,” amesema Rais huyo.
Katika hotuba yake, Rais Mwinyi pia aliwashukuru wasio Waislamu kwa mshikamano waliouonesha wakati wa mwezi wa Ramadhani, akibainisha kuwa ushirikiano huo unaimarisha ustahimilivu wa kidini nchini.
Kuhusu usalama wakati wa sikukuu, Rais Mwinyi ameziagiza mamlaka husika kuhakikisha ulinzi na usalama vinaimarishwa, hasa kwenye viwanja vya sikukuu na barabarani, ili kuepusha ajali zisizotarajiwa.
“Lazima tuhakikishe sheria za usalama barabarani zinaheshimiwa na watoto wanakuwa salama dhidi ya vitendo vyovyote vinavyoweza kuharibu amani na furaha yao,” amesisitiza.
Naye Ustadh Muhamed Suleiman Zuberi, akihutubia baraza hilo, alisisitiza kuwa mshikamano wa viongozi ni nguzo ya mafanikio ya taifa, huku akiwahimiza wananchi kuwatii viongozi wao kwa ajili ya kudumisha amani na maendeleo.
Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora, Haroun Ali Suleiman amesema kwa sasa kuna ushirikiano mkubwa kati ya Wizara yake na Ofisi ya Mufti na lengo ni moja tu kuhakikisha kila jambo linakwenda kwa amani nchini.
Viongozi waliohudhuria baraza hilo ni pamoja na Makamu wa Kwanza wa Rais, Othman Masoud, Makamu wa Pili wa Rais, Hemed Suleiman Abdulla, Spika wa Baraza la Wawakilishi, Zubeir Maulid na Jaji Mkuu wa Zanzibar, Khamis Ramadhan Abdalla.
Wengine ni pamoja na Rais wa Awamu ya Sita, Amani Abeid Karume, Rais wa Awamu ya Saba, Dk Ali Mohamed Shein na Makamu wa Pili wa Rais Tanzania mstaafu, Dk Gharib Bilal.