
Washington. Rais wa zamani wa Marekani, Joe Biden (82), amegundulika kuwa na ugonjwa wa saratani ya tezi dume, ambayo imesambaa hadi kwenye mifupa yake.
Saratani ni ugonjwa unaotokea pindi ukuaji wa seli mwilini unatokea katika namna isiyoweza kudhibitiwa na kuenea kwa kasi, kwa mujibu wa Shirika la Utafiti wa Magonjwa la Cancer Research UK.
Taarifa iliyotolewa jana Jumapili, Mei 18, 2025 kutoka ofisi ya Biden, imesema kiongozi huyo aliyeondoka madarakani Januari 2025, alibaini Ijumaa baada ya kuonana na daktari wiki iliyopita kutokana na dalili zilizojionesha katika njia ya mkojo.
Ofisi yake imeongeza kuwa saratani aliyokuwa nayo Biden haiathiriwi na homoni, hivyo inaweza kudhibitiwa.
Katika taarifa ya Jumapili, ofisi ya Biden imesema: “Siku ya Ijumaa, aligunduliwa na saratani ya kibofu, yenye alama ya Gleason ya 9 (Daraja la 5) na metastasis kwenye mfupa.”
Kutokana na taarifa hiyo, Rais Donald Trump ameandika kwenye mtandao wake wa kijamii wa ‘Truth Social’ kuwa yeye na mkewe, Melania Trump, “Tunasikitika kusikia kuhusu kilichobainika hivi karibuni wakati wa uchunguzi wa Joe Biden.”
“Tunatuma salamu zetu za heri kwa Jill na familia. Tunamtakia Joe ahueni ya haraka na yenye mafanikio.”
Kwa upande wake, Makamu wa Rais wa zamani Kamala Harris, aliyehudumu chini ya Biden, aliandika kwenye X kwamba yeye na mumewe, Doug Emhoff, wanaiweka familia ya Biden katika maombi yao.
“Ninatambua kuwa atapambana na changamoto hii kwa ustahimilivu na subira kutokana na sifa yake na kupambana na kuwa kiongozi wa mfano,” ameandika Harris.
Rais wa zamani, Barack Obama, naye alionyesha kuguswa na taarifa hiyo, amechapisha salamu zake kuwa: “Mimi na Michelle tunaiwazia familia ya Biden. Hakuna mtu ambaye amekuwa mstari wa mbele kupambana na ugonjwa wa saratani kama alivyofanya Biden, tunaamini hata hili atalishinda, tunamuombea apone haraka.”
Wakati huo, Rais wa zamani, Bill Clinton, ameandika kwenye mtandao wa X kuwa: “Rafiki yangu Joe Biden amekuwa mpambanaji siku zote. Mimi na Hillary tuko pamoja na familia yake sambamba na kutoa msaada kwa Jill wakati huu mgumu.”
Waziri wa Mambo ya Nje, Marco Rubio, naye ameandika: “Mimi na Jeanette (mkewe) tunaiombea familia ya Biden kwenye wakati huu mgumu.”
Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa mashirika ya habari.