Raia watatu wa Marekani wafutiwa hukumu ya kifo DRC, yumo mtoto wa Malanga

Kinshasa. Mahakama nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) imebatilisha hukumu ya kifo waliyopewa raia watatu wa Marekani kwa makosa ya jinai, ugaidi na kujaribu kuipindua serikali ya nchi hiyo.

Shirika la Habari la Reuters, limeripoti leo Aprili 2,2025, kuwa taarifa ya Ikulu ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) imeeleza watatu hao sasa hawatotumikia adhabu ya kifo badala yake watatumikia kifungo cha maisha jela.

Walikuwa miongoni mwa watu 37 waliohukumiwa kifo Septemba mwaka jana (2024) na Mahakama ya Kijeshi nchini DRC katika mashitaka hayo ambayo hata hivyo waliyakanusha.

Watatu hao ambao ni mtoto wa raia wa Marekani kwenye asili ya DRC (Christian Malanga), Marcel Malanga Malu, rafiki zake Tylor Thomson na Zalman Polun Benjamin, walipewa msamaha wa mtu binafsi kutoka kwa Rais Felix Tshisekedi.

Walishtakiwa kwa kuongoza genge la uhalifu lililotekeleza shambulio dhidi ya ikulu na makazi ya mshirika wa rais wa nchi hiyo, Mei, 2024.

Kubatilishwa kwa hukumu hiyo kunakuja kabla ya ziara ya mshauri mpya mwandamizi wa Marekani barani Afrika, Massad Boulos. Ambapo ziara hiyo imelenga kwenda DRC.

Boulos, ambaye ni mkwe wa Tiffany Trump, binti wa Rais wa Marekani, Donald Trump, anatarajiwa kuwasili Kinshasa Alhamisi Aprili 3, 2025, ambapo katika ziara hiyo mbali ya kuzuru DRC pia atafika Rwanda, Kenya na Uganda.

Marekani haijawatangaza Wamarekani hao watatu kuwa wamefungwa kimakosa katika magereza ya DRC, lakini Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilisema hapo awali kuwa kulikuwa na mazungumzo kati ya nchi hizo kuhusu suala hilo.

Kiongozi anayedaiwa kuwa wa mpango huo, Christian Malanga, ambaye ni raia wa Marekani mwenye asili ya DRC, aliuawa wakati wa shambulio hilo pamoja na watu wengine watano.

Kwa jumla, watu 51 walihukumiwa katika Mahakama ya Kijeshi, huku vikao vya kesi vikirushwa moja kwa moja kwenye televisheni na redio ya Taifa nchini humo.

Mbali na hao, watu 14 waliachiwa huru baada ya mahakama kubaini kuwa hawakuwa na uhusiano na shambulio hilo.

Hukumu za kifo hazijatekelezwa nchini DRC kwa takriban miongo miwili na wafungwa waliopokea adhabu hiyo kwa kawaida hutumikia kifungo cha maisha badala yake.

Serikali iliondoa marufuku hiyo mnamo Machi mwaka huu, ikitaja haja ya kuwaondoa wasaliti kutoka katika jeshi la taifa linalodaiwa kutofanya kazi ipasavyo. Hata hivyo, hakuna adhabu yoyote ya kifo iliyotekelezwa tangu wakati huo.

Msemaji wa Ikulu ya DRC, Tina Salama, akizungumza kupitia Televisheni ya taifa jana Jumanne, alisema Rais Tshisekedi alisaini maagizo ya kubatilisha adhabu ya kifo ya Wamarekani hao kuwa kifungo cha maisha.

Mmoja wa Mawakili wa Malanga, Ckiness Ciamba, aliliambia Shirika la Habari la Reuters kuwa “msamaha wa rais ni hatua ya kwanza inayoahidi mabadiliko makubwa katika siku zijazo.”

Mbali na hao, Raia wa DRC na  Ubelgiji, Jean-Jacques Wondo, aliyekuwa pia amehukumiwa kifo, alihamishiwa Ubelgiji Februari mwaka huu, kutokana na hali mbaya ya afya. Haijulikani kama Wamarekani hao pia watarejeshwa nyumbani kutumikia vifungo vyao ama la.

Pia haijulikani kama wafungwa wengine, wakiwemo raia wa Uingereza, Ubelgiji, na Canada, waliohukumiwa katika kesi hiyo watapunguziwa adhabu zao.

Jaribio la mapinduzi lilianza katika Mji Mkuu, Kinshasa, alfajiri ya Mei 19,2024, wakati washambuliaji wenye silaha waliposhambulia kwanza makazi ya spika wa Bunge, Vital Kamerhe, kisha kuelekea katika makazi rasmi ya rais.

Mashuhuda wanasema kundi la takriban washambuliaji 20 waliovaa sare za jeshi walishambulia Ikulu na mapigano ya risasi yakafuata dhidi ya Jeshi la DRC la FARDC kisha kuzidiwa na kuzingirwa. Baadaye walifikishwa mbele ya Mahakama ya Kijeshi na kupewa hukumu hiyo.

Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa mashirika ya habari.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *