
Raia wa Kenya wanaofanya kazi za ndani nchini Saudi Arabia wamekuwa wakitupwa jela, kubaguliwa na wakati mwingine kubakwa na waajiri wao, mazingira ya kazi yakiwa magumu kiasi cha kuwafanya kugeukia kazi ngumu au biashara ya binadamu, imesema ripoti ya shirika la Amnesty International.
Imechapishwa:
Dakika 1
Matangazo ya kibiashara
Ripoti hiyo inaelezea kwa undani, simulizi za wanawake wa Kenya waliorejea kutoka Saudi Arabia ambapo walikuwa wakisaidiwa na mashirika ya kibinadamu kutokana na ukatili waliokumbana nao.
Mara nyingi walilazimika kufanya kazi ngumu kwa mshahara mdogo, ambapo kwa mfano waliambiwa wangeajiriwa kama walimu, lakini walijikuta wakifagia, kupika na kutunza watoto.
Wakiwa kwenye nyumba za waajiri wao, wanawake walizuiwa kufanya mambo mengi ikiwemo kunyimwa faragha , hawakuruhusiwa kutoka nje isipokuwa wakiwa wameandamana na mwajiri huku wachache hawakuwahi kabisa kuruhusiwa kutoka nje.
Amnesty International inapendekeza, Saudi Arabia iwalinde wafanyakazi wa nyumbani chini ya sheria ya kazi kama inavyowalinda wafanyakazi wengine na kwa upande wa Kenya, ishirikiane na Riyadh kuweka mikakati ya usalama kwa wafanyakazi hao kabla ya kuondoka na wanapokuwa kazini.