
Wananchi wa Gabon wanajiandaa kupiga kura kesho kumchagua rais, katika uchaguzi wa kwanza katika nchi hiyo ya Afrika ya Kati, baada ya kutokea kwa mapinduzi ya kijeshi mwaka 2023.
Imechapishwa:
Dakika 1
Matangazo ya kibiashara
Siku ya Ijumaa ndio ya mwisho ya kufanya kampeni, ambapo wagombea wanane akiwemo kiongozi wa kijeshi anayeongoza serikali ya mpito, Brice Oligui Nguema ni miongoni mwa wagombea, wanaotafuta uongozi wa nchi hiyo.
Oligui Nguema, alikuwa amalize kampeni yake hivi leo, lakini aliamua kumaliza siku ya Alhamisi, akiahidi kurejesha demokrasia ya kweli katika nchi hiyo ya Afrika ya Kati yenye utajiri wa mafuta.
Mwezi Machi, kiongozi huyo wa serikali ya mpito, alitangaza kuwania urais katika uchaguzi huu, ambao utashuhudiwa na waaangalizi kutoka Umoja wa Afrika na Umoja wa Ulaya.
Mpinzani wa karibu wa Oligui Nguema, ni aliyekuwa Waziri Mkuu Alain Claude Bilie-By-Nze, ambaye ameahidi kuimarisha hali ya uchumi na kuunda nafasi za ajira hasa kwa vijana.
Uchaguzi wa Jumamosi, utamaliza miaka zaidi ya 50 ya familia ya Bongo ambayo imekuwa ikiongoza nchi hiyo, hadi alipoondolewa madarakani Ali Bongo Ondimba.